KANUNI SAHIHI ZA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI

Kaya nyingi hapa nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia chakula na kipato. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni pamoja na mayai, nyama, mbolea na manyoya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mifumo ya ufugaji kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria na shadidi. Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
• Kufuga kuku kwenye banda bora
• Kuchagua kuku bora wa kufuga
• Kutunza na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
• Kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuku
• Kutunza kumbukumbu

BANDA LA KUKU

Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
• Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
• Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
• Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
• Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala
• Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga
• Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji
• Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa
• Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga
Vifaa vinavyotumika kwa ujenzi wa banda
Vifaa vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
• Sakafu Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
• Kuta Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
• Paa Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
• Wigo Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati
Ukubwa wa banda
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina, na njia ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki 1 – 4. Hivyo banda lenye mita za mraba 16 linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki 4. Baada ya wiki 4 eneo hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na njia inayotumika katika ufugaji kama inavyoonekana kwenye Jedwali Na. 1
Jedwali Na 1: Eneo Linalohitajika Kufuga Kuku Kwenye Sakafu ya Matandazo Kutegemea na Umri na Aina ya Kuku
Umri wa kuku
Idadi ya kuku kwa mita 1 ya mraba
Kuku wa mayai
Kuku wa nyama
Siku 1 hadi wiki 4
18
18
Wiki ya 5 hadi ya 8
9
9
Wiki ya 9 hadi 20
6
Wiki 21 na kuendelea
3 – 4
Angalizo:
Mabanda yanayozungushiwa wigo kama ilivyo katika mfumo wa nusu huria, kuku mmoja huhitaji eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 10. Mfano, kuku 100 huhitaji eneo la mita za mraba 1000
Vifaa na Vyombo Muhimu
Mfugaji anashauriwa kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na kuboresha utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku. Vifaa na vyombo vinavyohitajika kwa ajili ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na kupumzikia vinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za mifugo. Aidha, mfugaji anaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye mazingira yake.

KUCHAGUA KUKU BORA WA KUFUGA

Kuku wa Asili
Aina za kuku wa asili wanaopatikana hapa nchini ni pamoja na Kuchi (Kuza), Poni (Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji). Mfugaji anaweza kuongeza uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa zifuatazo:-
• Uwezo wa kutaga mayai mengi (kati ya 15-20) katika mzunguko mmoja wa utagaji (Jedwali Na 2),
• Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi,
• Uwezo wa kustahimili magonjwa,
• Anayetoka maeneo yasiyo na magonjwa; na
• Umbo kubwa na kukua haraka.
Jedwali Na 2: Masuala ya Kuzingatia Wakati wa Kumchagua Kuku Mtagaji wa Kienyeji
Viungo vya mwili
Sifa
Macho
Maangavu, yenye wekundu kwa mbali na makubwa yamejaa kwenye soketi za macho.
Mdomo
Wenye rangi ya njano kwa mbali
Kisunzu/upanga
Chekundu, laini, kimelala kidogo upande na kinang’aa
Shingo
Iliyosimama
Umbali kati ya kidari na nyonga
Upana wa vidole 3-4 vya mpimaji
Upana wa nyonga
Upana wa vidole 3 vya mpimaji
Kuku wa Kisasa
Kuku bora wa kisasa kwa ajili ya mayai au nyama ni mwenye sifa zifuatazo:-
• Uwezo wa kuanza kutaga wakiwa na umri mdogo (miezi 5 – 6) kutegemea na koo,
• Umbo kubwa na anayekua haraka (kilo 1.5-2.0 kwa kipindi cha wiki 8-12) kutegemea na koo kwa kuku wa nyama,
• Anayetaga mayai mengi (250 au zaidi) kwa kuku wa mayai kwa mwaka; na
• Awe na uwezo wa kutaga katika umri wa miezi 6 – 8.
Kuchagua Jogoo Bora wa Mbegu
Jogoo wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:
• Achaguliwe kutoka kwenye koo zenye sifa ya kutaga mayai mengi,
• Mrefu, umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu,
• Awe machachari, ushawishi kwa mitetea na ari ya kupanda; na
• Uwezo wa kupanda akiwa na umri wa miezi 7 – 10.
Kuchi chotara
PITIA
AINA ZA MAGUGU NA MADAWA YA UDHIBITI
Mayai kwa Ajili ya Kutotoa Vifaranga
Uchaguzi wa Mayai
Mayai kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
• Yaliyorutubishwa na jogoo,
• Yasiwe na nyufa,
• Yasiwe na maganda tepetepe,
• Yasiwe na kiini kilichovunjika,
• Yawe na ukubwa wa wastani; na
• Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2 baada ya kutagwa.
Utunzaji wa Mayai
Mayai ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa kusimamishwa wima sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku 3 za mwanzo na kisha yageuzwe ili sehemu iliyo butu iangalie chini. Mayai yahifadhiwe kwenye sehemu iliyo na ubaridi kidogo na giza.

UTUNZAJI WA KUKU KWA MAKUNDI

Utunzaji wa Vifaranga
Malezi bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu vifaranga hawana uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara wanapoanguliwa. Ukosefu wa malezi bora husababisha vifaranga kuwa dhaifu, kufa kwa wingi na hivyo kupunguza idadi ya kuku wa baadaye. Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa kutumia kuku walezi au kutumia vifaa maalum.
Kulea Vifaranga kwa Kutumia Kuku Mlezi
Vifaranga wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku wengi wametotoa vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi aliye na uwezo wa kulea vifaranga wengi kati ya waliototoa aendelee kulea na wengine waliototoa waachwe huru ili warudi kwenye mzunguko wa kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga 20 hadi 25. Mfugaji wa kuku, pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia yafuatayo:-
• Kuku anayelea vifaranga atengewe chumba maalum, apewe maji ya kutosha na chakula chenye virutubishi muhimu,
• Vifaranga wasiachiwe kutoka nje hadi watakapofika umri wa wiki 6,
• Vifaranga watengwe na mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama aendelee na mzunguko wa kutaga; na
• Katika maeneo yenye hali ya hewa ya ubaridi vifaranga wacheleweshwe kutenganishwa na mama/malezi hadi wiki ya 6 au mpaka waonekane wameota manyoya ya kutosha.
Kulea Vifaranga kwa Kutumia Bruda
Bruda ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwapatia joto vifaranga badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga wengi kwa kutumia bruda ambayo ni mduara unaoweza kutengenezwa kwa kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa kuziba pembe za chumba. Aidha, njia hii hupunguza vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na ndege au wanyama hatari, huruhusu kuku kutaga mapema zaidi na kuwa na mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). Vilevile, hurahisisha udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa kutumia bruda:-
• Kuweka vifaa vya kuongeza joto kwa mfano taa ya umeme, chemli au jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto katika bruda kinachohitajika. Wiki ya kwanza ni 35 oC, wiki ya pili ni 33 oC, wiki ya tatu ni 31 oC na wiki ya nne ni 29 oC,
• Kuchunguza mtawanyiko wa vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini hali ya joto. Wakijikusanya kwenye chanzo cha joto, inaashiria kuwa baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa mbali na chanzo cha joto maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
• Bruda iwe na sakafu yenye malalo yatokanayo na maranda ya mbao au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe endapo yataonekana yameloana,
• Bruda iwekwe vifaa vya maji na chakula. Maji na chakula kiwekwe kabla ya kuweka vifaranga,
• Vifaa vya joto viwekwe ndani ya bruda masaa 6 kabla ya kuingia vifaranga,
• Vifaranga walishwe chakula cha kuanzia gramu 12 – 15 kwa kipindi cha wiki ya kwanza na gram 15 – 21 kwa kipindi cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21 – 35 kwa kifaranga na chakula hicho kiwepo muda wote,
• Vifaranga wapatiwe vitamini, madini na dawa za kinga (antibiotics); na
• Vifaranga wapatiwe chanjo kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa mifugo. Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu kwa mfano, Marek’s (mara anapototolewa), Mdondo (siku ya 3 – 4 na kurudiwa baada ya siku ya 21 na kila baada ya miezi 3) na Gumboro (siku ya 7 na kurudia tena siku ya 21). Wapatiwe dawa ya minyoo (wiki ya 8) na Coccidiosis (wiki ya 3 – 4)
Kutunza Kuku Wanaokua (wiki 8 – 18)
Utunzaji wa kundi hili unategemea mfumo unaotumika.
Kuku Wanaofugwa Katika Mfumo Huria
Kuku wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora yakiwemo yafuatayo;
• Wapewe chakula cha ziada asubuhi kabla ya kutoka na wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza kugawanywa mara 2 kwa siku,
• Wapatiwe maji safi na ya kutosha wakati wote; na
• Wapatiwe chanjo na dawa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Kuku Wanaofugwa Katika Mfumo Shadidi
• Majogoo watenganishwe na mitetea katika wiki 7 hadi 10 ili kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
• Wapewe chakula cha kukuzia kuanzia wiki ya 8 – 15 gramu 55 – 60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65 – 80 kwa wanaofugwa mfumo huria na gram 120- 125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa mfumo wa shadidi,
• Kuku wa nyama wapatiwe chakula cha kuku wa nyama muda wote,
• Wapatiwe maji safi ya kunywa kwa muda wote kwenye vyombo visafi,
• Kuku wachunguzwe dalili zozote za ugonjwa ili waweze kupata tiba sahihi kutoka kwa mtaalamu wa mifugo,
• Kuku wa wiki 9 – 20 wanahitaji nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa kuku,
• Kuwe na vyombo maalum vya kutosha kwa ajili ya chakula na maji
• Wafanyiwe usafi wa banda mara kwa mara ili kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu; na
• Wakatwe midomo ili kuzuia kudonoana.
Kuku Wanaotaga
Mahitaji ya kuku wanaotaga ni tofauti na ya makundi mengine. Mambo ya kuzingatia kwa kuku wanaotaga ni pamoja na:-
• Banda liwe na viota vya kutagia mayai (kiota 1 kwa kuku 3 – 5). Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha umri wa wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
• Wapatiwe chakula na maji safi wakati wote kwa kutumia vyombo maalum ambavyo ni visafi,
• Kuku wasiotaga waondolewe kwenye kundi. Kuku hao huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na kavu, upanga wake kichwani (comb) huwa mdogo na mwekundu,
• Wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3,
• Wawekewe fito au ubao mwembamba kama sehemu ya kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
• Mayai yakusanywe mara 4 au zaidi kwa siku ili yasidonolewe na kuku,
• Kuwe na malalo makavu na yabadilishwe mara yanapochafuka,
• Vyombo vifanyiwe usafi kila siku ili kuzuia magonjwa; na
• Watundikiwe majani mabichi aina ya mchicha, papai, alfaalfa, majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe.

UDHIBITI NA TIBA DHIDI YA MAGONJWA YA KUKU

Kuku wanaopata lishe bora, kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yanayotokea mara kwa mara huwa na afya nzuri. Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama. Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba. Kanuni muhimu za kufuata ili kuzuia magonjwa ni:-
• Banda liwe safi muda wote,
• Kabla ya kuweka kuku, banda linyunyiziwe dawa ya kuua wadudu wa magonjwa mbalimbali,
• Kuku wakaguliwe kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
• Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,
• Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
• Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,
• Banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine,
• Lango la kuingilia katika banda la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea vya wadudu wa magonjwa; na
• Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote.
Dalili za Kuku Mgonjwa
Dalili za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama zifuatazo:-
• Kuzubaa,
• Kupoteza hamu ya kula,
• Kujitenga na wenzake katika kundi; na
• Kupunguza au kusimama kutaga.
Mfugaji anapoona mojawapo ya dalili hizo amwone mtaalam wa mifugo

UFUGAJI WA AINA NYINGINE ZA NDEGE

Aina ya ndege wengine wanaofugwa hapa nchini ni pamoja na Bata maji, Bata bukini, Bata mzinga, Kanga na Njiwa. Ndege hao hufugwa kwa kiasi kidogo ukilinganisha na kuku kwa kuwa soko lao ni dogo. Utunzaji wao hautofautiani sana na kuku;
• Wajengewe banda la kuishi ambalo ukubwa wake utategemea idadi ya ndege wanaofugwa,
• Wapatiwe chakula chenye virutubisho na maji ya kunywa ya kutosha,
• Wapatiwe kinga na tiba dhidi ya magonjwa,
• Bata maji na Bata bukini wajengewe bwawa lenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuogelea; na
• Njiwa wajengewe viota sehemu ya juu kama kwenye mapaa ya nyumba.

UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU

Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ndege wengine wafugwao ili kusaidia mfugaji kujua maendeleo ya ufugaji wake. Utaratibu wa kuweka kumbukumbu mara tukio linapotokea ni lazima ili kuepuka kusahau. Mfugaji ahakikishe anaweka kumbukumbu ambazo ni sahihi na zinazoeleweka.
Aina za Kumbukumbu
Kumbukumbu zinazopaswa kuwekwa ni pamoja na:-
• Aina na idadi ya kuku waliopo kwenye kila kundi (mfano vifaranga, wanaokua, wanaotaga, majogoo),
• Uzalishaji wa mayai kwa kundi la kuku waliopo,
• Utotoaji wa vifaranga,
• Kinga na matibabu,
• Mapato na matumizi,
• Utagaji wa kila kuku na utunzaji (kwa kuku wa asili); na
• Kumbukumbu za vifo.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

Njoo ujifunze kilimo cha nyanya

NYANYA ni zao linalopendwa kutumiwa….kunogesha chakula, chakula kilichowekwa NYANYA huwa na radha nzuri inayomvutia mlaji Wakulima wengi hutamani kulima zao hili wengi huandika FAIDA na

Read More »

KILIMO BORA CHA KOROSHO

Korosho ni zao ambalo chimbuko lake ni Portuguese na baadae 16 century ndipo lilipo fika africa katika nchi ya msumbiji na baadae likafika nchini Kenya

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »