DUME ZURI KWA UZALISHAJI WA NG’OMBE WA MAZIWA

Tunaangalia uchaguzi wa dume mzuri kwa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, pamoja na aina ya malisho ambayo mfugaji anaweza kuyatumia kuweza kukabiliana na changamoto ya malisho kwa ng’ombe.

Wafugaji wengi wamekuwa wakipata ng’ombe wanaozalisha kidogo na kwa kiwango cha chini kutokana na kuangalia ukubwa wa gharama ya mbegu wakidhania kuwa ndiyo upatikanaji wa ng’ombe bora. Vinasaba husaidia kwa kiwango kikubwa katika kupata ng’ombe mzuri wa maziwa.

Kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa maziwa hutegemeana na vitu viwili ambavyo ni kuboresha mifugo kwa kufanya uchaguzi sahihi wa kizazi pamoja na usimamizi mzuri unaojumuisha lishe kamili, malazi mazuri, upatikanaji wa maji,kuwa karibu na wanyama pamoja na utoaji wa kinga na tiba dhidi ya magonjwa.

Vinasaba pamoja na usimamizi mzuri ni vitu viwili vinavyotegemeana. Bila kuwa na uzao mzuri, uzalishaji wa wanyama pamoja na usimamizi utakuwa wa hali ya chini sana, na bila usimamizi mzuri wanyama bora hawawezi kuonesha ubora wao katika uzalishaji.

Uzao mzuri humpa nafasi kubwa mfugaji kutambua sifa na uzalishaji utakaopatikana katika uzao ujao. Endapo mfugaji atafanya uchaguzi mbaya basi ni hakika atakuwa na uzalishaji hafifu wa maziwa, kuzorota kwa afya ya mnyama pamoja na maisha mafupi.

MUDA WA KUFANYA TAFITI
Wafugaji wengi wamekuwa wakifikiria mbegu pale tu ng’ombe anapokuwa tayari anahitaji kupandwa na matokeo yake ni kuwa, kutokana na haraka ya kutaka kumhudumia ng’ombe huyo, basi mfugaji atakuwa tayari kuchukua mbegu yoyote ile atakoyopatiwa na wataalamu.

Kwa mantiki hiyo, hakuna muda mfugaji atatumia kuchunguza aina ya dume aliyetumika kupatikana kwa mbegu hiyo na badala yake, gharama hutumika kwa kiasi kikubwa kuonesha uwezo wa dume huyo.

Wafugaji wengi hufikiri kuwa kitendo cha mbegu kuuzwa kwa gharama kubwa ni moja ya njia ya kutambua ubora wa dume. Wauzaji wengi wamekuwa wakitumia njia hii kuwadanganya na kuwarubuni wafugaji.

Ni muhimu sana kwa mfugaji anaelenga kuzalisha maziwa kusoma na kuelewa taarifa zote muhimu zilizotolewa kuhusu aina ya dume husika. Ili kufanikiwa katika uzalishaji wa maziwa, ni muhimu kwa mfugaji kuwa makini na kulichukulia kwa uzito suala la uchaguzi wa dume na kuelewa nini kinahitajika bila kubahatisha.

Mfugaji ni lazima atambue kuwa, dume huchangia asilimia 50 ya kinasaba katika uzao wake hivyo ni muhimu sana kujua sifa za dume unayemchukua kwa ajili ya uzalishaji. Pia ubora wa maziwa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya dume aliyetumika.

Dume wa maziwa hutambulika kwa kuangalia kiwango cha maziwa yanayozalishwa na ng’ombe aliyepandwa na dume huyo na mtamba aliyezaliwa na ng’ombe huyo ambapo dume huyo husambaza sifa ya maziwa kutoka kwa ng’ombe huyo hadi kwa mtamba.

ELEWA MAELEKEZO YALIYOPO KWENYE KABRASHA LA MBEGU
Kielelezo cha vinasaba hutumika kupima uwezo wa mnyama kusambaza vinasaba vyake kwenda kwa uzao ujao. Katalogi huwa na taarifa muhimu ambazo zitamsaidia mfugaji kufanya uchaguzi mzuri wa dume ili kuwa na uhakika wa kuendeleza kizazi baada ya kingine.

UPANDISHAJI
Mfugaji anapaswa kumpandisha ng’ombe kwa umri na wakati muafaka ili kuepuka matatizo ya uzazi na pia kuhakikisha anapata ndama bora na maziwa mengi.  Mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na

 1. Mtamba apandishwe akiwa na umri wa miezi 17 -24 na uzito wa kilo 230 – 300 kwa ng’ombe wa kigeni na umri wa miezi 30 – 36 na uzito wa kilo 200 kwa ng’ombe wa asili.  (Rejea jedwali Na 2)
 2. Ng’ombe aliyekwisha zaa apandishwe siku 60 baada ya kuzaa na
 • Siku 18 – 23 baada ya kupandishwa, ng’ombe achunguzwe kama ana dalili za joto ili apandishwe tena.  Iwapo ng’ombe ataendelea kuonyesha dalili za joto baada ya kupandishwa mara tatu mfugaji apate ushauri wa mtaalam wa mifugo.
PITIA
UFUGAJI WA BORA WA BATA MZINGA

JEDWALI NA.2.  UMRI NA UZITO UNAOSHAURIWA KUPANDISHA MTAMBA

AINA YA NG’OMBE UZITO (KG) UMRI (MIEZI)
Friesian 240 – 300 18 – 24
Ayrshire 230 – 300 17 – 24
Jersey 200- 250 18 – 20
Mpwapwa 200 – 250 18 – 20
Chotara 230 – 250 18 – 24
Boran 200 – 250 24 – 36
Zebu 200 30 -36

DALILI ZA NG’OMBE ANAYEHITAJI  KUPANDWA
 Ni muhimu mfugaji akazitambua dalili za ng’ombe anayehitaji kupandwa ili aweze kumpandisha kwa wakati.  Dalili hizo ni pamoja na

 • Kupiga kelele mara kwa mara
 • Kutotulia/kuhangaika
 • Kutokwa na ute mweupe usiokatika ukeni
 • Kupenda kupanda wenzake na husimama akipandwa na wenzake na
 • Kunusanusa ng’ombe wengine

Ng’ombe akionyesha dalili za joto apandishwe baada ya masaa 12, kwa kuhimilisha au kwa kutumia dume bora (kwa mfano, akionyesha dalili asubuhi apandishwe jioni na akionyesha dalili jioni apandishwe asubuhi).

UHIMILISHAJI
Uhimilishaji ni njia ya kupandikiza mbegu kwa ng’ombe jike kwa kutumia mrija.  Faida za uhimilishaji ni pamoja na kusambaza mbegu bora kwa haraka na kwa gharama nafuu, kupunguza gharama za kutunza dume na kudhibiti magonjwa ya uzazi.

ILI MFUGAJI ANUFAIKE NA HUDUMA HII ANAPASWA KUFANYA YAFUATAYO:-

 • Kuchunguza kwa makini ng’ombe mwenye dalili za joto
 • Kumjulisha mtaalam wa uhimilishaji mapema ili kuwezesha zoezi hili kufanyika kwa wakati.
 • Kuchunguza kama ng’ombe atarudi kwenye joto siku ya 18 – 23 baada ya kupandishwa na
 • Ng’ombe aliyepandishwa apimwe mimba siku 60 hadi 90 baada ya kupandishwa.

MATUNZO YA NG’OMBE MWENYE MIMBA
Ng’ombe mwenye mimba huchukua miezi 9 hadi kuzaa.  Katika kipindi hicho chote anastahili kupatiwa lishe bora na maji ya kutosha ili akidhi mahitaji ya ndani aliye tumboni na kutoa maziwa mengi baada ya kuzaa.

Mambo ya kuzingatia ni pamoja na

 • Ng’ombe apewe lishe bora na maji ya kutosha kipindi chote cha mimba
 • Miezi 2 kabla ya kuzaa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku
 • Apewe kinga dhidi ya maambukizi na tiba ya magonjwa
 • Ng’ombe anayekaribia kuzaa, hususani mtamba, azoeshwe kuingia kwenye sehemu ya kukamulia.

DALILI ZA NG’OMBE ANAYEKARIBIA KUZAA
Mfugaji anapaswa kufahamu dalili za ng’ombe anayekaribia kuzaa ili aweze kufanya maandalizi muhimu.  Dalili hizo ni pamoja na

 • Kujitenda kutoka kwa wenzake
 • Kiwele kuongezeka
 • Chuchu kutoa maziwa zikikamuliwa
 • Kutokwa na ute mwekundu na sehemu za uke kuvimba na kulegea
 • Kuhangaika kulala chini na kusimama na
 • Kati ya saa moja hadi mbili kabla ya kuzaa sehemu ya uke hutokwa na maji mengi ambayo husaidia kulainisha njia ya ndama kupita.

HUDUMA KWA NG’OMBE ANAYEZAA
Ng’ombe anayezaa anahitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha usalama wa ng’ombe na ndama anaezaliwa.  Mambo ya kuzingatia ni pamoja na yafuatayo:-

 • Sehemu ya kuzalia ng’ombe iandaliwe kwa kuwekwa nyasi kavu na laini na iwe safi.
 • Ng’ombe ahamishwe sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuzaa mara baada ya dalili za kuzaa kuonekana na
 • Ng’ombe aachwe azae mwenyewe bifa usumbufu
PITIA
MATUMIZI YA UHAKIKA YA DAWA ZA KUDHIBITI VIUMBE HAI TEGEMEZI WA MIFUGO

MFUGAJI  APATE  USHAURI/HUDUMA  KUTOKA  KWA  MTAALAM  IWAPO MATATIZO  YAFUATAYO  YATAJITOKEZA:-

 • Ng’ombe kushindwa kuzaa kwa masaa mawili hadi matatu baada ya chupa kupasuka
 • Kondo la nyuma kushindwa kutoka masaa sita baada ya kuzaa
 • Kizazi kutoka nje na
 • Ng’ombe kushindwa kusimama baada ya kuzaa

MATUNZO YA NG’OMBE ANAYEKAMULIWA
Ng’ombe anayekamuliwa anahitaji kupata chakula kwa ajili ya kujikimu na cha ziada kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa.  Ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa maziwa ng’ombe

 • Apewe chakula cha ziada kwa kiwango cha kilo 1 kwa kila lita 2 – 3 za maziwa anayotoa.
 • Apewe madini na virutubisho vingine kulingan ana mahitaji
 • Apewe maji mengi kwa vile ni ya muhimu katika kutengeneza maziwa.
 • Aachwe kukamuliwa siku 60 kabla ya kuzaa.  Uachishwaji huu ufanywe taratibu ili ifikapo siku ya 60 kabla ya kuzaa ukamuaji usitishwe.
 • Baada ya kusitisha kukamuliwa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku hadi atakapozaa na
 • Apatiwe kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa na tiba kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.

UZALISHAJI WA MAZIWA
Lengo la ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi na salama pamoja na mazao yatokanayo na maziwa .

Mambo muhimu ya kuzingatia ni:-

 • Sehemu ya kukkamulia iwe safi na yenye utulivu
 • Ng’ombe awe na afya nzuri msafi na kiwele kioshwe kwa maji safi ya uvuguvugu.
 • Mkamuaji  awe msafi kucha fupi na asiwe na magonjwa ya kuambukiza
 • Inashauriwa mkamuaji asibadilishwebadilishwe
 • Vyombo vya kukamulia viwe safi
 • Muda wa kukamua usibadilishwe na
 • Maziwa ya mwanzo kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza ugonjwa wa kiwele.

UNENEPESHAJI WA NG’OMBE WA NYAMA
Ng’ombe kwa ajili ya nyama anaweza kuchinjwa akiwa na umri wa kuanzia miezi 3 kulingana na mahitaji ya soko.  Kwa kawaida hapa Tanzania ng’ombe huchinjwa wakiwa na umri wa kuanzia miezi 18 kwa ng’ombe wa kigeni na zaidi ya miezi 36 kwa ng’ombe wa kigeni na zaidi ya miezi 36 kwa ng’ombe wa asili.

Ili mfugaji aweze kupata faida kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa nyama anapaswa afanye yafuatayo:-

 • Afuge aina ya ng’ombe wanaokua na kukomaa haraka
 • Anenepeshe ng’ombe kwa muda wa miezi 3 – 6 kabla ya kuchinjwa.  Unenepeshaji huongeza ubora wa nyama na kipato kwa mfugaji.
 • Awapatie chakula chenye mchanganyiko wenye viinilishe vya kutosha viinilishe vya kutia nguvu na joto mwilini viwe na uwiano mkubwa kuliko vingine (Jedwali Na.3), na
 • Auze ng’ombe mara wanapofikisha umri na uzito unaohitajika katika soko ili kuepuka gharama za ziada.

JEDWALI NA.3. MFANO WA MCHANGANYIKO WA CHAKULA KWA AJILI YA UNENEPESHAJI

AINA YA CHAKULA KIASI KWA KILO
Majani makavu ya mpunga/NganoHey 23.3
Molasis 44.72
Mahindi yaliyorazwa 18.94
Mashudu ya Alizeti/pamba 11.4
Madini mchanganyiko 0.7
Chumvi 0.47
Urea 0.47
Jumla 100

UZALISHAJI NA UHIFADHI WA MALISHO BORA NA VYAKULA VYA ZIADA
Chakula kikuu cha ng’ombe ni nyasi, vyakula vingine ni pamoja na miti malisho, mikunde na mabaki ya mazao.  Ili kupata malisho misimu yote ya mwaka ni muhimu kuvuna na kuhifadhi malisho kipindi yanapopatikana kwa wingi.

Inawezekana kupanda malisho mengi kuliko kiasi kinachohitajika msimu mmoja/wakati wa mvua, kuyavuna yanapofikia hatua ya kutoa maua na kuyahifadhi (mfano wa malisho yanayoweza kupandwa ni mabingobingo, Guatemala, African fox-tail, desmodium, centrosema, lukina n.k).  Malisho yakupandwa ni vizuri yawe na mchanganyiko wa jamii ya nyasi, mikunde na miti malisho.

PITIA
UFUGAJI WA KISASA WA NG’OMBE

MASALIA YA MAZAO SHAMBANI
Masalia ya mazao shambani kama vile mabua, magunzi, majani ya mikunde, viazi, ndizi, mpunga, na mengineyo yanaweza kukusanywa na kuhifadhiwa vizuri kama chakula cha ng’ombe.

MALISHO YA MITI NA MATUNDA YAKE
Malisho yatokanayo na miti ya malisho na matunda yake yanaweza kutumika kama malisho ya ng’ombe.  Majani na matunda ya miti ya lukina, sesibania, migunga na mbaazi yanaweza kukaushwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kulisha ng’ombe.

VYAKULA VYA ZIADA
 Ili kukidhi mahitaji ya viinilishwe kulingana na kiwango cha uzalishaji, ng’ombe anatakiwa kupewa vyakula vya ziada.  Vyakula hivyo vinatokana na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali.  Michanganyiko hii  inategemeana na upatikanaji wa malighafi katika maeneo husika.  Mifano ya mchanganyiko huo ni kama ifuatavyo:-

JEDWALI NA. 4  MFANO WA KWANZA WA CHAKULA CHA ZIADA

AINA YA CHAKULA KIASI (KILO)
Pumba za mahindi 47
Mahindi yaliyoparazwa 20
Mashudu ya alizeti/pamba 20
Unga wa lukina 10
Chokaa ya mifugo 2
Chumvi 1
Jumla 100

Mfugaji anatakiwa kuzingatia yafuatayo ili kupata tija katika ufugaji:-

 • kulisha mchanganyiko wa nyasi, mikunde na mchanganyiko wa madini na vitamin
 • kutenga maeneo kwa ajili ya kulisha ng’ombe kwa mzunguko pamoja na kupanda malisho katika mfumo huria na nusu huria na
 • kuvuna nyasi na mikunde inapofikia hatua ya kutoa maua na kuyahifadhi kwa matumizi wakati wa uhaba wa malisho hususan wakati wa kiangazi.

NJIA ZA KUHIFADHI MALISHO
Malisho yanaweza kuhifadhiwa kwa kuyakausha (Hei) au kuyavundika (Sileji).

HEI: Hei ni majani yaliyohifadhiwa kwa kukaushwa baada ya kukatwa au kuachwa kukauka yakiwa shambani kwa matumizi ya baadaye.  Katika kutengeneza hei yafuatayo yazingatiwe:-

 • vuana malisho yanapoanza  kutoa maua
 • Yaanikwe kwa siku 3 hadi 6 kutegemea aina ya malisho na hali ya hewa na yageuze mara 1 au 2 kwa siku ili yakauke vizuri.
 • Yafungwe katika marobota baada ya kukauka inawezekana kutumia kasha la mbao lenye vipimo vifuatavyo:-  Urefu sentimeta 75, upana sentimeta 45 na kina sentimeta 35 au mashine na zana za kufunga marobota ya hei na
 • Hifadhi marobota juu ya kichanja ili kuzuia maji yasiingie unyevu na kuharibiwa na wadudu.

SILEJI: Sileji ni majani yaliyokatwakatwa na  uvundikwa.  Madhumuni ya kuyavundika ni kuyawezesha kubaki na ubora wake hadi wakati yatakapotumika katika kutengeneza sileji yafuatayo yazingatiwe:-

 • Tengeneza sileji kwa kutumia majani yenye sukari nyingi kama mahindi au mabingobingo na mikunde, mabaki ya viwandani kama molasis,
 • Andaa shimo au mfuko wa plastiki kulingana na kiasi cha majani yaliyovunwa.
 • Vuna majani ya kuvundika katika umri wa kuanza kutoa maua.  Endapo majani yaliyovunwa ni teketeke yaachwe kwa siku moja yanyauke kupunguza kiwango cha maji.
 • Katakata majani uliyovuna katika vipande vidogovidogo,
 • Tandaza majani uliyokatakata ndani ya shimo au mfuko katika tabaka nyembamba na kushindilia ili kuondoa hewa yote.
 • Funika shimo ulilojaza majani kwa plastiki ikifuatiwa na udongo.
 • Sileji itakuwa tayari kutumika kuanzia siku 21 na
 • Sileji iliyofunguliwa kwa ajili ya matumizi ifunikwe haraka iwezekanavyo ili kuzuia kuharibika. Sileji inaweza kubaki na ubora katika shimo kwa muda mrefu kama haitafunguliwa na kuachwa wazi kwa muda mrefu.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

Udongo

KAZI YA KILIMO TANZANIA.

Watu wengi kwenye vyombo vya habari wanalalamika maranyingi wakiwemo vijana, wazee na watu wa umri wa kati kuwa hakuna kazi. Je, hivi nikweli kuwa hakuna

Read More »

KILIMO BORA CHA KAROTI

UTANGULIZI Karoti ni zao la mbogamboga ambalo ni zao mzizi, kwa kawaida hupatikana katika rangi ya machungwa, zambarau, nyeusi, nyekundu, nyeupe na njano. Karoti za

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »