JIFUNZE NAMNA YA KUTENGENEZA MBOLEA YA MBOJI

Mboji ni nini?
Mboji ni aina ya mbolea ya asili yenye rangi nyeusi na harufu nzuri ya kidongo ambayo hutokana na kuoza kwa mchanganyiko wa masalia ya mimea kunakosababishwa na vijidudu na wadudu rafiki wa mazao.  
Muozo wa kutengeneza mbolea ya mboji ni tofauti na muozo wa kawaida kwa sababu muozo wa mboji unahitaji usimamizi ili kupata matokeo mazuri ambapo masalia ya mimea mbalimbali (ambayo kwa pamoja hutambulika kama malighafi) hukusanywa na kutengeneza biwi au lundo litakalooza na kuwa mboji kamili.
Je ulishawahi kutumia mbolea ya mboji? Jibu laweza kuwa ndio. Lakini Je unajua jinsi ya kuandaa mbolea ya mboji? Kama ulikuwa unajiuliza swali hili basi umefika mahali sahihi. Hapa utajifunza hatua kwa hatua jinsi ya kutengeneza mbolea ya mboji.

VITU VYA MSINGI KATIKA KUTENGENEZA MBOLEA YA MBOJI

Vijidudu na Wadudu
Sehemu kubwa ya lundo la mboji huozeshwa na vijidudu kama vile bakteria na fangasi ambavyo katika hali ya unyevu huitaji Kaboni (C) kama chanzo cha nishati na Naitrojeni (N) kama kiungo muhimu cha protini, amino acid na enzymes muhimu kwa ukuaji wa seli zao na kuzaliana. Hii ina maana kwamba ili vijidudu vinavyoozesha mboji viweze kuongezeka na kufanya shughuli za kibailojia huitaji malighafi vyanzo vya Kaboni na malighafi vyanzo vya Naitrojeni katika uwiano mzuri.
Vilevile baadhi ya wadudu rafiki wa mazao huhusika katika kumeng’enya malighafi wakati wa kutengeneza mboji. Wadudu hao ni kama vile jongoo, tandu, mnyoo mwekundu, kiwavi wa bito, siafu n.k.
Uwiano wa Malighafi

Wadudu wanaohusika katika uozeshaji wa malighafi katika biwi
Hewa
Vijidudu huitaji hewa ya oksijeni ili viweze kuozesha malighafi kwa muozo unaohitaji hewa (aerobic decomposition). Katika kiwango cha kutosha cha hewa ya oksijeni vijidudu huzaliana kwa kasi na hivyo biwi huoza kwa haraka. Vilevile hewa ya Carbon dioxideinayozalishwa kutokana na kuoza kwa malighafi inahitajika kutolewa nje ya biwi. Hivyo Kama unataka kutengeneza mboji kwa haraka hunabudi kuhakikisha biwi linakuwa na mzunguko mzuri wa hewa.
Unyevu
Vijidudu vinahitaji unyevu ili viweze kuishi na hivyo kuozesha malighafi kwa urahisi. Shughuli za kibaiolojia za vijidudu zinaweza kusimama ikiwa biwi litakuwa katika hali ya ukavu uliopitiliza. Vilevile biwi linapokuwa limelowana sana hudidimia na kuzuia kuingia kwa hewa na hivyo kupelekea kutokea kwa muozo husiohitaji hewa (anaerobic decomposition).
Joto
Joto huchochea shughuli za kibaiolojia za vijidudu na kusafisha biwi kwa kuua mbegu za magugu na vimelea vya magonjwa vilivyo katika malighafi. Kiwango kikubwa cha joto huongezeka katika biwi kutokana na shughuli za kibaiolojia zinazofanywa na vijidudu katika kuozesha malighafi na kiwango fulani kutokana na mionzi ya jua.
AINA ZA MUOZO WA MBOJI
Biwi /Lundo la mboji huweza kuoza kwa namna mbili: Muozo unaohitaji hewa na Muozo usiohitaji hewa.
 • Muozo Husiohitaji Hewa (anaerobic decomposition)
Huu ni muozo unaosababishwa na vijidudu ambavyo havitegemei hewa kuozesha malighafi katika biwi la mboji.  Kukosekana kwa hewa ya oksijeni katika biwi kunaweza kupelekea kutokea kwa muozo huu ambapo matokeo yake huwa ni kutengenezwa kwa tindikali lacticna butyric kunakopelekea mboji inayotengenezwa kuwa katika hali ya kitindikali.
Muozo huu pia husababisha lundo la mboji kutoa harufu mbaya inayotokana na gesi yaAmmonia na Hydrojen sulphide zinazozalishwa wakati wa mchakato wa kuoza kwa malighafi. Joto linalozalishwa kutokana na muozo huu kwa kawaida halizidi nyuzi joto za sentigredi 45 hivyo mbegu na mizizi ya magugu, vimelea vya magonjwa na waduduhuendelea kuishi katika mboji.
Matumizi ya mboji ya Muozo usiohitaji hewa
Matumizi ya mbolea ya mboji inayotokana na muozo huu yanahitaji taadhari kwa kuwa yanaweza kusababisha kuongezeka kwa hali ya tindikali katika udongo na hivyo kuathiri mazao hasa pale inapotumika katika udongo wenye hali ya kitindikali. Inashauriwa kutumia mboji hii pale kunapokuwa na ufahamu wa kiwango sahihi cha tindikali katika udongo wa shamba.
 • Muozo Unaohitaji Hewa (aerobic decomposition)
Muozo huu hufanywa na vijidudu vinavyotumia hewa ya oksijeni kuozesha malighafi zilizo katika lundo la mboji. Muozo huu husababisha kutengenezwa kwa mbolea ya mboji iliyo katika hali ya kati (neutral). Tofauti na Muozo usiohitaji hewa matumizi ya mbolea ya mboji inayotokana na muozo huu hayahitaji taadhari yoyote inayohusu kuathiri tindikali ya udongo au mazao. Kwa sababu hiyo, katika makala hii nitakueleza jinsi ya kutengeza mbolea ya mboji inayotokana na muozo huu.
MALIGHAFI NA VIFAA MUHIMU
Malighafi Mbichi
Malighafi mbichi hujumuisha majani mabichi, mashina ya kijani ya mimea na mabaki ya jikoni kama vile maganda ya mboga mboga na matunda yaliyooza.  Malighafi mbichi huwekwa katika lundo kama chanzo cha Naitrojeni (N). Mfano: Majani ya mimea ya jamii ya mikunde, magugu mabichi, nyanya zilizooza, maganda ya kabichi, maganda ya ndizi, nyasi changa zisizo na mbegu, maganda ya kahawa, majani ya mlonge, majani ya muembe n.k.
Malighafi mbichi

Malighafi mbichi za majani mabichi na mabaki ya jikoni
Malighafi kavu
Malighafi kavu hujumuisha majani yaliyokauka ya mimea mbalimbali, vijiti na mabaki makavu ya mazao. Malighafi kavu huwekwa katika biwi kama chanzo cha Kaboni (C). Mfano; Mabua ya mahindi, mabua ya mtama, mabua ya mpunga, majani makavu yaliyo pukutika kutoka katika miti, magugu yaliyokauka, nyasi kavu, vijiti, makaratasi, maranda ya mbao n.k.
Malighafi kavu

Malighafi kavu zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa mboji
Malighafi za ziada
Malighafi za ziada zinazoweza kutumika katika utengenezaji wa mboji hujumuisha samadi, mboji iliyotayari, na udongo wa juu wa ardhi ya shamba linalolimwa. Malighafi hizi zote hutumika kama chanzo cha vijidudu vya kuozesha lundo la mboji. Vile-vile majivu pia huweza kutumika kurekebisha kiwango cha tindikali katika lundo.
Vitu visivyotakiwa katika biwi
Baadhi ya vitu haviitajiki kuwekwa katika biwi kama malighafi. Vitu hivyo ni kama vifuatavyo;
 1. Mimea au mabaki ya mazao yaliyonyunyiziwa madawa ya viuatilifu hivi karibuni.
 2. Mabaki ya nyama, maziwa, samaki au vyakula vyenye mafuta ambayo huvutia panya, nzi na vimelea vya magonjwa na kusababisha biwi kutoa harufu mbaya.
 3. Mimea au sehemu za mimea yenye miba mikali.
 4. Mizizi ya magugu sugu.
Vifaa na Vitendea kazi
Vifaa na vitendea kazi vinavyohitajika katika kutengeneza biwi ni kama vile;
 1. Maji huhitajika kwa ajili ya kuongeza unyevu katika biwi/lundo la mboji.
 2. Koleo na jembe huitajika kwa ajili kuchimbia mashimo.
 3. Uma wa shambani au Koleo kwa ajili ya kugeuzia biwi.
 4. Miti mirefu kwa ajili ya kusimikia kichanja na kupima joto la biwi.
 5. Nyasi kwa ajili ya kufunikia kichanja cha biwi.
 6. Kamba au Tape measure kwa ajili ya kufanyia vipimo.
 7. Chombo cha kunyunyizia maji au Water cane
 8. Toroli kwa ajili ya kubebea malighafi

HATUA ZA KUTENGENEZA MBOLEA YA MBOJI

Zifuatazo ni hatua unazotakiwa kufuata katika maandalizi ya mboji:
 • Uchaguzi wa eneo
Kwa utengenezaji wa mboji chagua eneo linaloweza kufikika kwa urahisi karibu na shamba au bustani ambapo mboji inayotengenezwa itaenda kutumika. Vile-vile eneo hilo liwe na upatikanaji mzuri wa maji au liwe karibu na chanzo cha maji.
 • Maandalizi ya eneo
Baada ya kuchagua eneo lisafishe kwa kuondoa magugu, mawe na kung’oa visiki kama vipo. Pima eneo lenye upana wa m 1.5 na urefu wowote utakaopendezwa nao kisha chimba mashimo mawili au zaidi kwa kufuatana yenye urefu wowote na kina cha sm 25 hadi 50.
Hali ya hewa ya eneo husika huzingatiwa katika uchimbaji wa mashimo ambapo kwa kadili eneo lilivyo kame ndivyo kina cha mashimo kinavyopaswa kuwa kirefu. Kama eneo ulilochagua halina kivuli jengea kichanja juu ya eneo la kutengenezea mboji katika kimo cha mita 3 hadi 5.
 • Ukusanyaji wa malighafi
Ni vyema kukusanya malighafi kutoka mimea tofauti kwa sababu kila mmea huwa na kiwango tofauti cha Kaboni na Naitrojeni. Hata hivyo aina na kiwango cha malighafi hutegemea upatikanaji wa malighafi husika mahali ulipo. Hivyo tumia malighafi zilizopo katika eneo lako kwa kiwango unachoweza kumudu kutegemeana na mahitaji.
 • Maandalizi ya Malighafi
Malighafi ziandaliwe kwa kuzikatakata ili kupunguza ukubwa na kuzifanya ziweze kuoza kwa urahisi katika lundo la mboji. Hili lifanyike hasa kwa malighafi kubwa au ngumu kama vile mabaki ya mazao kama mabua ya mahindi au mtama ambayo yanapaswa kupunguzwa hadi kufikia urefu wa sm 10 hadi 15. Vile-vile malighafi ndefu kama nyasi unaweza kuzikata nusu ya urefu wake ili zisikusumbue wakati wa kupanga matabaka katika lundo.
kibanda cha mboji

Eneo lililoandaliwa kwa ajili ya utengenezaji wa mboji
 • Uandaaji wa Lundo la Mboji: Uwiano wa Malighafi
Inashauriwa kuweka malighafi mbichi na malighafi kavu kwa kiasi kinachofanana katika lundo la mboji. Kwa mfano ikiwa utatumia majani mabichi na majani makavu kama malighafi pekee katika lundo la mboji unaweza kuweka kiasi cha debe mbili za majani mabichi na debe mbili zingine majani makavu.
 • Kupanga Matabaka
Lundo la mboji huandaliwa kwa kupanga malighafi kwa mtindo wa matabaka hadi kufikia kimo cha m 1 hadi 2 kwenda juu. Matabaka ya malighafi hupangwa kwa mpangilio hufuatao;
 1. Mwagia maji au kandika udongo kuta na pembe zote za shimo kisha weka malighafi ngumu kama vile mabua ya mahindi au mtama na vijiti au vitawi vya miti katika shimo kutengeneza tabaka la msingi lenye unene wa sm 15 hadi 25. Tabaka hili husaidia kuwepo kwa mzunguko mzuri wa hewa katika lundo. Nyunyizia maji juu ya tabaka la msingi ili liwe na unyevu.
 2. Weka malighafi kavu zinazooza kwa urahisi kama vile majani makavu ya miti au nyasi kavu laini juu ya tabaka la msingi kutengeneza tabaka la kwanza lenye unene wa sm 20 hadi 25 kisha nyunyizia maji.
 3. Weka malighafi mbichi kutengeneza tabaka la pili lenye unene wa sm 20 hadi 25. Usinyunyizie maji juu ya tabaka hili.
 4. Weka samadi au mabaki ya mboji ya zamani kutengeneza tabaka la tatu lenye unene wa sm 2 kisha nyunyizia maji.
 5. Weka udongo wa juu kutengeneza tabaka la nne lenye unene wa sm 2 hadi 3.
 6. Nyunyizia kiasi kidogo cha mkojo au majivu au vyote kwa pamoja juu ya lundo kuharakisha uozaji wa malighafi.
 7. Weka malighafi kwa kurudia mpangilio huu wa matabaka kwa kurudia tabaka la kwanza, la pili, la tatu na la nne hadi lundo litakapofikia kimo kinachopendekezwa.
 8. Chomeka mti mrefu uliochongoka wenye unene wa angalau sm 2 katika biwi kwa ajili ya kukagulia joto. Miti ya mianzi hupendelewa sana kwa kazi hii kwa sababu ina uwezo wa kupitisha hewa kuingia na kutoka katika biwi.
HATUA ZA KUOZA KWA BIWI LA MBOJI
Muozo wa mboji hupitia katika awamu tatu tofauti hadi kupata mboji yenyewe ambayo ni matokeo ya kuoza kwa mabaki ya mimea kama ifuatavyo;
 • Awamu ya Joto (Thermophilic phase)
Hii ni awamu inayoanzia siku tatu za mwanzo tangu kutengenezwa kwa lundo ambapo joto katika lundo la mboji hupanda hadi kufikia nyuzi joto za sentigredi 60 hadi 70 hasa sehemu za katikati. Joto jingi katika awamu hii ni matokeo ya shughuli za kibaiolojia zinazofanywa na vijidudu aina ya bakteria vinavyoweza kuhimili joto jingi (thermophilic bacteria) katika kumeng’enya malighafi zilizo katika lundo.
Malighafi nyingi zinazoozeshwa katika awamu hii ni zile laini kama vile majani mabichi, maganda ya mboga, majani makavu ya miti n.k. Kutokana na fukuto la joto katika awamu hii vimelea vinavyosababisha magonjwa, wadudu waharibifu, mbegu na mizizi ya magugu hufa na hivyo mboji huwa safi. Awamu hii hudumu kwa siku kadhaa au hata mwezi kutegemeana na malighafi zilizotumika, hali ya hewa na sababu nyinginezo.
 • Awamu ya Kupoza (Mesophilic phase)
Hii ni awamu ambapo joto la lundo hushuka hadi kufikia nyuzi joto za sentigredi 40 hadi 45 na wakati mwingine huweza kufikia nyuzi joto za sentigredi 25. Katika awamu hii vijidudu aina ya fangasi huusika zaidi ambapo malighafi ngumu kama vile vijiti, majani makavu, mashina ya mimea na mabua huozeshwa. Awamu hii huchukua wiki kadhaa na wakati mwingine ni vigumu kuitofautisha na awamu ya kupevuka.
 • Awamu ya Kupevuka (Maturation phase)
Katika awamu hii wadudu rafiki wa mazao kama vile jongoo na tandu huusika katika kumalizia mmengenyo wa malighafi zilizo katika lundo. Vile-vile katika kuoza kwa malighafi katika awamu hii uyoga unaweza kuota katika biwi. Mwishoni mwa awamu hii lundo la mboji hupungua hadi kufikia nusu ya lilivyo kuwa awali.
MATUNZO YA BIWI LA MBOJI
Matunzo ya biwi la mboji uhusisha unyunyiziaji maji, ugeuzaji wa biwi na kudhibiti joto kama ifuatavyo;
 • Kunyunyizia Maji
Biwi/Lundo linatakiwa kunyunyiziwa maji mara mbili kwa wiki ili kufanya liwe na unyevu unaohitajika. Kujua kwamba biwi linahitaji kuongezwa maji utafanya jaribio la kuweka fungu dogo la nyasi kavu katikati mwa lundo kwa kupenyeza kupitia pembeni kwa muda wa dakika tano na kisha kulitoa. Ikiwa hata baada ya kulitoa fungu hilo ukakuta bado ni kavu elewa kwamba kiwango cha unyevu katika biwi hakitoshi na hivyo kuna haja ya kuongeza maji katika biwi. Endapo utakuta fungu hilo lina majimaji au unyevu usiongeze maji katika biwi.
Kumwagilia mboji

Unyunyiziaji wa maji katika biwi
(Photo credit; the organic farmer.org)
Zingatia: Hakikisha unanyunyizia maji katika biwi hadi linapokuwa na unyevu unaostahili kwa ajili ya kuoza kwa malighafi na si kulilowanisha sana.
 • Kugeuza /Kupindua biwi
Ni muhimu kupindua biwi kwa sababu husaidia kuingia kwa hewa safi katika biwi na kuoza kwa malighafi zilizokuwa nje au pembezoni mwa biwi. Wakati wa kugeuza biwi chota malighafi zote katika shimo la kwanza na kuzihamishia katika shimo linalofuata ukianza na malighafi za juu hadi kufikia chini kisha nyunyizia maji kama unyevu ni mdogo au ongeza nyasi kavu ikiwa malighafi zimelowana sana.
Biwi ligeuzwe kwa mara ya kwanza baada ya wiki mbili au tatu tangu kutengenezwa kisha kila baada ya wiki tatu hadi malighafi zitakapokuwa zimeoza vizuri.
 • Kudhibiti joto
Weka utaratibu wa kukagua na kufuatilia joto la biwi mara kwa mara kwa kipindi chote cha uozaji wa malighafi katika biwi. Ni muhimu pia kuhakikisha ndani ya siku tatu za mwanzo tangu kutengeneza lundo joto linakuwa juu kwa kadili iwezekanavyo si chini ya nyuzi joto za sentigredi 55 ili kuua mbegu za magugu na vimelea vya magonjwa katika biwi. Hili litawezekana ikiwa utaweka malighafi katika uwiano unaopendekezwa na kuzingatia matunzo ya biwi.
Ukaguzi wa joto katika biwi huweza kufanyika kwa kutumia kipima joto au mti uliouchomeka wakati wa kutengeneza lundo. Chomoa mti kutoka katika lundo kisha shika sehemu iliyokuwa imezama katika lundo na ikiwa sehemu hiyo ya mti itakuwa imepata joto ni kiashiria kwamba mchakato wa kuoza kwa malighafi umeanza lakini ikiwa haijapata joto tafsiri yake ni kwamba malighafi hazijaanza kuoza.
Kumbuka: Muozo wa biwi hupitia katika awamu tatu zenye joto tofauti hivyo basi joto unaloweza kuhisi katika mti wakati wa ukaguzi litaendelea kupungua taratibu hadi kwisha kabisa kuashiria mabadiliko ya awamu za muozo kutoka awamu moja kwenda nyingine.
Kukagua mboji

Jinsi ya kukagua joto katika biwi kwa kutumia mti
MATATIZO YANAYOWEZA KUJITOKEZA KATIKA BIWI LA MBOJI
SN Tatizo Sababu Suluhisho
1 Biwi kutoa harufu mbaya kama ya yai lililooza. Kiwango kidogo cha hewa au maji kuwa mengi katika biwi. Geuza biwi kisha ongeza malighafi kavu ngumu.
2 Biwi kushindwa kupata joto au kuoza taratibu (i) Kiwango kidogo cha Naitrojeni katika biwi (ii) Biwi ni dogo (iii) Kiwango kidogo cha unyevu katika biwi (iv) Kiasi kidogo cha hewa (v) Kiasi kidogo cha maji katika biwi (i) Ongeza malighafi mbichi au nyunyizia mkojo wa mnyama (ii) Ongeza malighafi (iii) Geuza biwi na kisha nyunyizia maji (iv) Geuza biwi (v) Pindua biwi kisha nyunyizia maji
3 Harufu kali ya gesi ya Ammonia Kiwango kingi cha Naitrojeni katika biwi Ongeza malighafi kavu
PITIA
FAIDA ZA UTUMIAJI SAMADI MASHAMBANI


 

KUIVA KWA MBOLEA YA MBOJI
Muda wa Kuiva kwa Mboji
Mboji huwa tayari kwa matumizi baada ya mwezi mmoja hadi miezi kumi na mbili kutegemeana na ukubwa wa malighafi zilizowekwa katika biwi, kiwango cha matunzo ya biwi na matumizi ya mbolea ya mboji yaliyokusudiwa.
Viashiria vya Mbolea ya Mboji kuiva
Dalili zifuatazo katika lundo zinaweza kutumika kama viashiria vya kuiva kwa mboji;
 1. Lundo kusinyaa hadi kufikia nusu ya ukubwa wake wa awali.
 2. Malighafi ulizoziweka katika lundo zimeoza vizuri na hauwezi kuzitambua.
 3. Lundo limepoteza joto kabisa.
 4. Mboji yenye rangi nyeusi na harufu nzuri ya kidongo.
Jaribio la Kuiva kwa Mbolea ya Mboji
Ikiwa kwa kutumia viashiria unashindwa kuwa na uhakika wa kuiva kwa mboji yako unaweza pia kufanya jaribio hili dogo kwa kufuata hatua zifuatazo;
 1. Weka mboji katika viriba au tengeneza tuta dogo lenye ukubwa wa mita 1 ya mraba kwa kutumia mboji pasipo kuchanganya na udongo wowote.
 2. Panda kiasi cha mbegu 100 za nyanya katika viriba au tuta la mboji kisha hudumia kwa kumwagilia maji na kukagua miche kwa muda wa mwezi mmoja.
 3. Ikiwa hata baada ya mwezi mmoja umebakiwa na miche ya nyanya angalau sabini na tano yenye afya na majani ya kijani katika viriba au tuta basi jua fika mboji yako imeiva na iko tayari kwa matumizi.
Zingatia: unaweza kutumia mbegu za zao lolote katika kufanya jaribio hili cha msingi kagua afya ya miche ukizingatia rangi ya majani na mashina hadi itakapokuwa imekomaa na hakikisha unajua dalili za magonjwa yanayoshambulia zao husika.
Ushauri: Ikiwa una mashaka na mboji yako na kufanya jaribio hili unaona vigumu basi ni vyema kutumia mbolea ya mboji yako kama matandazo.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

Kilimo cha Maharage

Donec odio. Quisque volutpat mattis eros. Nullam malesuada erat ut turpis. Suspendisse urna nibh, viverra non, semper suscipit, posuere a, pede.

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »