Kilimo-Biashara ni neno moja linalo unganishwa na maneno mawili neno KILIMO na neno BIASHARA, na inaweza kuelezewa kuwa ni shughuli ya kilimo inayo husisha matumizi bora ya elimu ya ujasiriamali katika kujipatia faida. Katika hili nimuhimu sana kuzingatia mambo kadha wa kadha na ni kiini cha mafundisho ya nyaraka hii, kuwa watu wanatakiwa wafuate mbinu, teknolojia za kisasa na kwa faida. Inahusisha matumizi ya gharama ndogo katika uzalishaji ili kupunguza tatizo la ukata wa fedha na uchumi uliopo kulinda usiyumbe.
Kilimo ni shughuli ya kiuchumi ya uzalishaji mazao shambani, misituni, pamoja na ufugaji wa wanyama. Kilimo kina maana pana inayo husisha mifumo ya uzalishaji mazao ya mimea, misitu, ufugaji wa wanyama (kama mbuzi, kondoo, ngombe), samaki, ndege (kama kuku, bata na njiwa) n.k.
Watu wengi hujihusisha katika kilimo kwa namna moja au nyingine hasa kwa nchi zinazo endelea.Wapo wale wanaolima mazao kwaajili ya kupata chakula. Na kundi la pili ni wale wanao lima au kufuga kwa ajili ya biashara. Yote hayo ni kwaajili ya kujipatia kipato na kuishi maisha yaliyo bora zaidi. Hapa ni pamoja na kupata chakula, malazi, mavazi, elimu, maji na mambo mengine muhimu kwa binadamu kuishi vizuri.
“Kilimo sio sekta tuu ambayo inasaidia kukua kwa uchumi wa nchi barani afrika, lakini lazima iwe sekta tegemezi kwa ukuaji wa uchumi wa nchi za afrika”
(Paul Kagame- Rais wa Rwanda)

Biashara
Maana yake ni kuuza na /au kununua ili kujipatia faida na kukidhi matakwa ya mteja na matarajio. Zipo biashara nyingi duniani zinzfanyika, mfano: Biashara halali na zisizo halali kutegemea na sheria na taratibu za eneo au serikali husika. Biashara haramu zinzweza kuhusisha shughuli ambazo serikali imekataza kama kuuza na kununua madawa ya kulevya kama pombe haramu, konyagi, viroba, mirungi, gongo, bangi, kokeine na mengineyo madawa ya kulevya.
Zipo pia biashara nzuri sana na halali kabisa ambazo zinawaingizia watu kipato duniani kama biashara ya madini, biashara ya nguo, mazao, bidhaa mabali mbali za viwandani kama magari, ndege, meli, mashua, Computer na vitu vingine vingine vingi ambavyo mnaviona kwenye maduka, viosk, super market, hotel, stationary na mahali mahali.
Ushauri mzuri ili kufanikiwa ni kuwa watu wajihusishe na biashara halali ambao si kikwazo kwa jamii, serikali na kwa Mungu aliye iumba mbingu na nchi. Zile biashara za magendo na ambazo hasiko rasmi zinaweza kuonekana zinakuingizia kipato lakini mtu asipo kuwa makini anaweza kujikuta ana ingia gharama marambili au zaidi kutokana na faini na mambo kama hayo.
Kuipenda kazi yako ni kuithamini na kuilinda. Mtu yeyote ambaye anakitu chake cha thamani pale nyumbani si rahisi kumkuta anakiacha nje ovyo na hasa kama nyumba haina geti na ulinzi wa kutosha. Hii inaonyesha kuwa vitu vya thamani vinahitaji kulinda kupendwa na kuthaminiwa kama dhahabu na lulu vilivyo.
Ujasiriamali sasa ni nini?
Kuna wanaoelezea kuwa ni mbinu au mikakati au ushawishi wa muuzaji kwa kumtaka mnunuzi anunue bidhaa au huduma hata kama mnunuzi alikuwa hana wazo na nia ya kununua ili huyo muuzaji apate faida (Salim, F.R).
Kwa ujumla ujasiriamali ni hali ya kutumia ushawishi, ubunifu, akili ya ziada na uwezo binafsi ilikufanikiwa kufanya jambo fulani katika maisha kwa kutumia vizuri fursa zilizopo. Sio lazima ujasiriamali uwe kwenye biashara, ujasiriamali unaweza kuwa katika kilimo, ujasiriamali kwenye matumizi ya fedha za mikopo mashuleni kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na mambo mengine mengi ya kimaisha ili kupata faida.
Kusudi la Ujasiriamali.
❖ Kujiajiri
❖ Kukuza kipato
❖ Kusaidia jamii katika kutoa huduma za jamii
❖ Kupata faida na mafanikio kwa ujumla.
❖ Kukuza ubunifu na vipaji binafsi
❖ Kuongeza furaha na uhuru katika kujipangia majukumu
❖ Kutumia muda vizuri
❖ Uwekezaji na kukuza ndoto katika maisha
❖ Kuondoa umaskini
❖ Kuondoa utumwa wa fikra na mawazo finyu.
Faida za ujasiriamali
❖ Kupata faida
❖ Kutumia vizuri rasilimali mbalimbali pamoja na karama zetu
❖ Kusaidia makundi ya watu wasiojiweza
❖ Kuwezesha miradi mingine ya kiuchumi
❖ Kuboresha mahusiano kati ya watu, jamii na serikali kwa ujumla.
Vikwazo katika ujasiriamali
❖ Ukosefu wa mtaji na teknolojia ya kutosha
❖ Elimu juu ya ujasiria mali
❖ Woga katika biashara
❖ Masoko ya bidhaa
FAIDA ZA KILIMO-BIASHARA
Ajira.
Kilimo kinatoa fursa ya mtu kujiajiri mwenyewe, kuajiriwa au kuajiri watu. Wapo wataalamu wanaoajiriwa kutokana na fani zao ili kutoa ushauri wa kitaalamu (consultancy), kufundisha, utafiti au ajira kwa vibarua wa kawaida kufanya shughuli za uzalishaji shambani n.k. Takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 65 ya watu wanapata ajira kwenye kilimo moja kwa moja au kupitia njia nyingine (indirect). Hivyo kuna fursa kwasababu watu wanahitaji chakula kwaaajili ya kula, kuuza au kulisha wanyama (kuku, nguruwe, njiwa na wengineo). Hii ni fursa nyeti kwa wahitimu wa shule za sekondari na vyuo wanao kaa bila kufanya kazi kwasababu hawajapata ajira rasmi na wanasubiri kuajiriwa.
Pato la taifa hasa la ndani (GDP).
Pamoja na mambo mengine, kilimo hasa kilimo biashara kinasadia sana kukuza pato la ndani kwa kulipa kodi kwa serikali. Wakulima wanapo lima kwa ajili ya biashara wanalipa kodi, lakini wanapolima kwa ajili ya chakula au matumizi binafsi huwa maranyingi hawalipi kodi. Hivyo watu wakilima kibiashara, wenyewe wanafaidika lakini na serikali inanufaika kupitia kodi. Kwa Tanania, kilimo kinachangia asilimia 30% kwenye pato la ndani GDP, 2016. KILIMO BIASHARA KINALIPA!!!
Kukua kwa biashara.
Kilimo biashara ni shughuli ambayo inakuza biashara kwa ujumla wake. Biashara iwe ya bidhaa kutoka sehemu nyingine nje ya kilimo au kutoka shambani kama matunda, mbogamboga, nafaka au mazao ya biashara kama pamba au mkonge vinakuwa kwa sababu ya kilimo-biashara. Bila kilimo biashara, biashara nyingi zina dorora. Mathalani, wapo wafanyabiashara wengi ambao mtaji wao unatokana na faida toka kwenye kilimo, kukopesha wakulima au biashara yenyewe ni mazao ya kilimo.
Kukua kwa viwanda
Malighafi zinazo hitajika viwandani mara nyingi, hasa kwa nchi zinazo endelea kama Tanzania zinatoka kwenye shambani-kwenye kilimo. Kwahiyo, kwenye kuendeleza viwanda nilazima kuongeza nguvu ya uzalishaji kwenye kilimo. Mazao yatokanayo na kilimo yawe ya kutosheleza mahitaji ya viwanda na mahitaji ya watu kama chakula na vitu vingine. Pamoja na kuongeza uzalishaji, kuna sababu pia ya msingi kuangalia na kuzingatia ubora wa bidhaa. Ili kuzingatia hili, wakulima wapate elimu na waifuate tangia hatua za awali katika kulima, mbolea, palizi, ukuzaji, uangalizi, usafirishaji, upakiaji au uhifadhi mpaka mlaji husika apate mzigo katika myororo wa bidhaa husika.
Kupatikana kwa chakula
Faida nyingine kubwa sana ya kilimo-biashara ni kupatikana kwa chakula. Ni wazi kwamba, sio watu wote ni wakulima. Wapo watu wanafanya kazi ofisini au mazingira ya mijini na hawa gusi jembe. Kimsingi, wanalimiwa na wakulima wengine, wao wana nunua chakula. Kama ni mahindi, mchele, ndizi, maharagwe na mazao mengine. Katika hili, kuna mwingine anaweza akalima na kuuza ili aweze kununua chakula na mahitaji mengine. Mathalani, mazao yake yalikuwa ya biashara.
Kuondoa/kupunguza umaskini.
Kuna njia nyingi za kuondoa, au kupunguza umaskini kwa jamii au serikali. Mbinu moja wapo ni kupitia kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya muhimu mfano chakula kwa njia mbadala. Kulima, kunampa mtu ujasiri wa kuwa na chakula cha kutosha siku za usoni. Wakulima wakibarikiwa kuvuna kama hakuna magonjwa ya kutisha msimu huo, mvua ni za kutosha na mambo ya msingi yapo sawasawa, inawezekana wakavuna na kupata ziada hivyo kupunguza umaskini na ukata na kuishi maisha bora.