KILIMO BORA CHA UFUTA

UTANGULIZI
Ufuta (simsim/sesame) ni zao la kibiashara ambalo mbegu zake zina kiasi kikubwa cha mafuta kiasi cha asilimia 45 hadi 55.Na zao hili linaweza kulimwa maeneo mengi ya Afrika mashariki  na Tanzania.Ni zao ambalo linatowa mafuta yenye thamani kubwa na hivyo kulifanya zao bora la biashara.

Ufuta (sesamum indicum) ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa na Mbeya. Zao hili hulimwa kwa ajili ya chakula na biashara. Mbegu za zao hili huwa na wastani wa mafuta kiasi cha asilimia 45.

Kwa sasa soko la ufuta Tanzania ni zaidi ya mara tatu ya uzalishaji wake, kwa mantiki hiyo zao hili lina soko kubwa sana. Uzalishaji wake unafanyika kwa kiasi kidogo kwa sababu wakulima wamekuwa wakilima zao hili la ufuta kwa mazoea na kutumia mazao yake kama nafaka ya kutengeza vyakula mbalimbali kama kashata. Lakini kama utalima kibiashara ni zao ambalo linaweza kukomboa jamii yetu kutoka katika dimbwi la umasikini

HALI YA HEWA  INAYOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA
Zao hili linawezwa kulimwa katika maeneo yanayopata mvua kidogo.Maeneo ya ukanda wa chini  usawa wa bahari hufaa zaidi kwa kilimo cha ufuta.Pia nyanda za juu ambazo ni chini ya mita 1500 hufaa kwa kilimo cha ufuta.Mfano kwa Tanzania unaweza Ukalima ufuta katika mikoa ya Morogoro,Lindi,Manyara,Dodoma,Iringa.

UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA
Ufuta ustawi vizuri katika maeneo yenye udongo mwepesi mweusi na usiotuamisha maji,udongo tifutifu ni mzuri kwa kilimo cha ufuta,Pia ufuta unawezwa kulimwa katika udongo wowote lakini usiotuamisha maji.Ufuta hufa haraka kama maji yatatuama kwa muda mrefu shambani.

AINA ZA UFUTA
Kuna aina kuu mbili za mbegu za ufuta:
1) MBEGU ZA ASILI
Wakulima wengi hupanda mbegu za asili, mbegu ambazo zilianza kulimwa miaka mingi iliyopita.Mbegu hizi nyingi zina mavuno kidogo na huchukua muda mrefu kukomaa Huchukua siku 140 hadi 180.

2) MBEGU ZA KISASA
Mbegu hizi zinakomaa kwa muda mfupi na hutowa mavuno mengi, wastani wa kilogram 500 hadi 800 kwa ekari kama shamba litaandaliwa litapandwa na litatunzwa vizuri.Mbegu hizi huchukua siku 105 hadi 140 kukomaa.Mfano wa mbegu hizi ni Naliendele 92,Lindi 202,Ziada 94 na Mtwara 2009.

UPANDAJI WA UFUTA
Shamba la ufuta ni budi likatuliwe na kulimwa vizuri kabla ya kupanda,hata hivyo pia unaweza kupanda bila kukatua lakini mavuno yatapungua kidogo.Inashauriwa kupanda ufuta kwa mistari kwa vipimo vifuatavyo.Sentimeta 50 kwa 10 au 50 kwa 20 kama utapanda kwa kutumia mistari ya kuchimba vijifereji vidogo katika mstari na kudondosha mbegu hizo katika vifereji hivyo (Drilling method) na kwa kuacha mche mmoja mmoja kwa kila shina.

Pia sentimeta 50 kwa 30  au 60 kwa 30 kwa kuacha miwili kwa kila shina. Kwa Mbegu ya Asili Unaweza Kupanda kwa sentimeta 70 kwa 30 kwa Kuacha Miwili kwa Kila shimo.Fukia mbegu kwa sentimenta .2.5 hadi 5.

PITIA
KILIMO BORA CHA MAPAPAI

MUDA WA KUPANDA
Muda mzuri wa kupanda ufuta ni mwanzoni mwa msimu wa kilimo  yaani Mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati kwa mwezi Januari.

MATUMIZI YA MBOLEA
 Ufuta ni zao ambalo halihitaji matumizi makubwa ya Mbolea.Japokuwa hustawi zaidi katika udongo wenye rutuba ya kutosha.Kama utapanda katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha basi unaweza kutumia mbolea kiasi kidogo Mbolea kama vile UREA na BUSTA.

MATUNZO NA PALIZI
Miche ya ufuta ni midogo na laini sana hivyo inahitaji palizi mapema hasa katika kipindi cha majuma manne ya kwanza .Pia katika kipindi hiki unatakiwa kupunguza miche iliyosongamana.Kadri utavyochelewesha palizi na kupunguzia mimea mapema ndivyo unavyoifanya mimea isikuwe vizuri na kujipunguzia kipato chako.

MAGONJWA YA UFUTA
Magonjwa makuu ya ufuta ni madoa ya majani na kuoza matawi na shina.Zuia magonjwa haya kwa Kupanda  mbegu bora  na kwa kutokupanda ufuta katika ardhi inayotuamisha  maji,pia itawezekana kubadilisha shamba usilime  ufuta katika shamba lililolimwa msimu uliopita.

WADUDU WANAOSHAMBULIA UFUTA
Kuna wadudu wengi wanaoshambulia ufuta kama vile vibaruti (Ambao hushambulia hatua ya mwanzo kabisa ya miche iliyoota ya ufuta  ambapo vibaruti hula majani ya mwanzo ya mmea mara tu yanapojitokeza).Pia Aphidi hushambulia ufuta kwa kufyonza maji katika majani ya mimea hivyo kupelekea kukauka kwa majani ya mmea.

Pia wapo funza wa majani ambao hula majani ya mimea na pia hufunga majani ya ncha ya mimea na kuzuia ukuaji wa matawi wa mimea,wadudu hawa ni hatari zaidi kwani wanazuia kutengenezwa kwa vitumba vya ufuta.

Kuzuia vibaruti,kabla hujapanda mbegu yako changanya na dawa ya tunza au gaucho.Pia panda mbegu bora na fanya mzunguko mazao shambani.Wadudu wengine wakijitokeza tumia dawa kama karate,dimethoate.Twigathoate,duduall,duduba  na dawa nyingine za wadudu kabla wadudu hawajasababisha madhara makubwa shambani.

 MAANDALIZI KABLA YA KUVUNAKAGUA SHAMBA
• Kagua shamba kuona kama ufuta umekomaa. • Ufuta hukomaa, kati ya miezi mitatu na minne tangu kupanda kutegemea aina.
• Aina ya ufuta usiokuwa na matawi hukomaa mapema kuliko ile yenye matawi.
• Ni muhimu kuwahi kuvuna ili kuepuka ufuta kupukutikia shambani.

  DALILI ZA KUKOMAA UFUTA SHAMBANI
• Kwa kawaida majani hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya manjano na hatimaye kudondoka.
• Mashina hubadilika rangi kutoka kijani na kuwa ya kahawia.

 VIFAA VYA KUVUNIA
• Kamba
• Siko
• Panga

  VIFAA VYA KUKAUSHIA
• Sehemu ya kukaushia yenye Sakafu ya saruji
• Maturubai
• Sakafu safi

USAFIRI
• Mikokoteni
• Matela ya matrekta
• Magari

  KUVUNA
• Vuna ufuta mapema kabla mapodo kukomaa sana na kuanza kupasuka na kuachia punje.Mapodo ya ufuta yaliyokomaa sana yakiguswa au kutikiswa na upepo hupasuka na kuachia mbegu, hali inayosababisha upotevu mkubwa.
• Mbegu za ufuta ni ndogo na zikidondoka chini ni vigumu kuziokota. Vilevile mbegu zilizodondoka ni vigumu kuzitenganisha na uchafu.
• Uvunaji wa ufuta huhusisha ukataji wa mimea yenye mapodo kwa kutumia vyombo vya mkono kama panga kwa kukata mashina.
• Kwa aina za ufuta zenye mapodo yanayopasuka, uvunaji ufanyike wakati mimea bado ni kijani ili kuepuka upotevu wa mbegu.
• Aidha uvunaji ufanyike wakati hakuna upepo wala jua kali.
• Baada ya kukata mashina yafunge katika mizigo midogo na kuweka katika vyombo vya kusafirisha kama vile mikokoteni, matela au magari hadi sehemu ya kukaushia.
• Panga mizigo midogo kwa kusimamisha katika malundo madogo yasiyozidi mizigo minane kwenye sehemu safi za kukaushia.

KUKAUSHA
Mapodo ya ufuta hukaushwa yakiwa yamefungwa katika vitita. Vitita huwekwa kwa kuegeshwa kwenye fremu ya kukaushia kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutegemea hali ya hewa. Fremu hii huwekwa juu ya turubai au sakafu ili kuzuia upotevu wa punje kutokana na kupasuka kwa mapodo.

PITIA
MAGONJWA MAARUFU YA SUNGURA

KUPURA
Upuraji hufanyika kwenye turubai, mkeka au kwenye sakafu safi.
• Vitita hupigwa taratibu kwa kutumia mti au hutikiswa vikiwa vimegeuzwa vichwa chini ili kuruhusu punje za ufuta kudondoka kwenye sakafu safi au turubai.

KUPEPETA NA KUPEMBUA
Kupepeta na kupembua hufanywa ili kuondoa takataka kama vile mawe, vipande vya mapodo,vijiti na vumbi.Njia bora ya kupepeta na kupembua ni kwa kutumia mikono.
• Ufuta huwekwa kwenye vyombo kama vile ungo kwa kiasi cha kilo mbili hadi tatu. Ufuta hurushwa hewani kwa kasi ndogo na takataka nyepesi huchukuliwa na upepo. Zile nzito huondolewa kwa mikono.

KUFUNGASHA
Mbegu za ufuta zilizo safi huwekwa kwenye vifungashio kama vile magunia madogo ya aina ya juti ya ujazo wa kilo 50.
• Fungasha mbegu za ufuta kwenye magunia yenye uzito usiozidi kilo 50. Kabla ya kufungasha hakikisha mbegu zimekauka hadi kufikia unyevu wa asilimia 10.

KUHIFADHI
• Panga magunia ya ufuta juu ya chaga.
• Panga kwa kupishanisha ili kuruhusu mzunguko wa hewa kati ya magunia.

KUSINDIKA MBEGU ZA UFUTA
Ufuta husindikwa kupata bidhaa ya mafuta ambayo hutumika katika mapishi mbalimbali. Mafuta hukamuliwa kwa kutumia njia za asili na kwa kutumia mashine. Njia za asili zina ufanisi mdogo ukilinganisha na zile za kukamua kwa mashine, hivyo ni vyema kutumia mashine. Kuna mashine za aina mbili zinazotumika kukamua mafuta; mashine za mkono na zile zinazoendeshwa kwa injini au mota ya umeme. Mashine za mikono zinazotumika zaidi hapa nchini ni za aina ya daraja (Bridge press) na Ram.

KUKAMUA KWA MASHINE YA DARAJA
Mashine ya daraja ni moja ya mashine za kisasa zinazoweza kukamua mafuta ya ufuta. Mashine hizi huendeshwa kwa mikono na zina uwezo wa kukamua mafuta kwa asilimia 68 hadi 72. Inaweza kukamua kilo 25 za ufuta kwa saa moja. Ili kupata ufanisi mzuri wa mashine hii, ni muhimu ufuta uwe na unyevu wa kati ya asilimia 11 na 13. Iwapo unyevu utakuwa chini ya kiwango hicho inashauriwa kunyunyizi maji kwenye ufuta kabla ya kukamua.

PITIA
MYCOTOXINS NI MOJA YA CHANGAMOTO KATIKA UZALISHAJI KUKU

 VIFAA VYA KUKAMULIA MAFUTA
• Mashine ya daraja
• Sufuria • Vifungashio
• Mifuko midogo ya nguo au viroba vyenye upana wa sentimita 20 na urefu wa sentimita 20.
• Chombo cha kukinga mafuta.
• Chujio safi
• Lebo
• Lakiri Malighafi
• Mbegu za ufuta safi
• Maji safi

  UKAMUAJI MAFUTA
• Nyunyuzia maji kidogo kwenye ufuta ili kuongeza unyevu kufikia asilimia 11 hadi 13. Mafuta hutoka vizuri kwenye kiwango hicho cha unyevu.
• Jaza ufuta kwenye vifuko vya nguo au viroba
• Vipange vifuko hivyo kwenye silinda na kuanza kuzungusha mhimili hadi mafuta yaanze kutoka kupitia matundu ya silinda.
• Acha kwa muda mafuta yaendelee kutoka kisha endelea kuzungusha mhimili hadi mafuta yaishe. Mhimili ukiacha kuzunguka ni dalili kuwa mafuta yamekwisha.
• Kusanya mafuta, chuja na fungasha kwenye chupa safi zilizochemshwa. Hakikisha chupa ni kavu na zina mifuniko.
• Weka lebo na lakiri
• Hifadhi mahali pakavu na pasipo na mwanga mkali.

   UKAMUAJI
• Anika mbegu za ufuta juani kwa kuzitandaza kwenye mabati ili zipate joto la kutosha.
• Lengo la kuanika mbegu juani ni kurahisisha ukamuaji wa mafuta.
• Jaza mbegu za ufuta kwenye mpare wa kulishia
• Funga wenzozuia (HANDLE)ili mbegu za ufuta zisitoke.
• Nyanyua wenzozuia mpaka juu ili kuruhusu mbegu za ufuta kuingia kwenye silinda.
• Shusha wenzozuia chini ili kuruhusu pistoni kusukuma mbegu za ufuta ziingie ndani ya eneo la shindilio
. • Nyanyua tena wenzozuia mpaka juu na kushusha na wakati huohuo ukiendelea kujaza mbegu za ufuta kwenye mpare wa kulishia. Wenzoinua ukiwa mzito ni dalili kuwa msukumo wa kutosha umejengeka. Msukumo huo utasababisha mafuta kutoka.
• Mafuta yanapoanza kutoka legeza wenzozuia ili kuruhusu mashudu kutoka.
• Chuja na hifadhi mafuta kwenye vyombo safi vyenye mifuniko vilivyochemshwa.

MASHINE ZA MOTA YA UMEME
Kwa wale wanaohitaji mashine za kukamulia mafuta zinazotumia mota za umeme wakiwa Dar es salaam wafike mtaa wa Nkuruma karibu na clock tower, pale kuna maduka kadhaa yanayouza mashine na zana mbalimbali za kilimo

  MATUMIZI
Mafuta ya ufuta hutumika katika mapishi mbalimbali ili kuongeza ladha. Pia husaidia kuleta nguvu na joto mwilini. Mbegu za ufuta huchanganywa na vyakula mbali mbali kama mikate, keki, mboga na kadhalika

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

Umwagiliaji wa Matone

Umwagiliaji wa matone ni mfumo wa kisasa kwa umwagiliaji wa mimea na hasa mazao. Maji hupelekwa polepole kwa mabomba au mipira yenye matundu madogo moja

Read More »

Kilimo Bora Cha Bilinganya

Bilinganya  imo  katika   jamii   ya  mimea   inayohusisha   nyanya,  pilipili,  viazi  mviringo  na  nyanya  mshumaa.    Mboga  hii  ina   viini lishe

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »