Kilimo ni moja ya sekta muhimu sana hasa kwa taifa ambalo bado ni changa na lina uhitaji wa kufanya mapinduzi ya viwanda na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wa Tanzania kilimo kinatajwa kuwa uti wa mgongo na asilimia kubwa ya watanzania ni wakulima. Japokuwa kilimo kinatajwa kuwa uti wa mgongo bado kinafanyika kwa kutumia teknolojia ya zamani na kumfanya mkulima kutopata tija kwenye kilimo.
Changamoto za kilimo Tanzania ni nyingi sana mfano matumizi ya teknolojia ya zamani, kutegemea kilimo cha mvua na kukosa uhakika wa soko.
Kwa miaka mingi iliyopita tumeshuhudia mapinduzi ya kilimo yakifanyika sehemu mbali mbali duniani na mapinduzi haya sana sana ni kwenye teknolojia ya kilimo. Hapa nazungumzia matumizi ya mashine kwenye kilimo pamoja, mbegu bora na viuatilifu ili kudhibiti magonjwa. Lakini jambo hili kwa Tanzania imekuwa ni changamoto kubwa sana hasa ukizingatia kuwa wakulima wengi ni wale wa hali ya chini ambao hawawezi kukidhi gharama zinazohitajika kuwekeza kwenye teknolojia mpya ya kilimo.
Changamoto nyingine ni kutegemea kilimo cha mvua. Hii inaathiri mkulima kwa kuwa msimu ambao mvua ni chache au hakuna mvua kabisa mazao yanakufa shambani hivyo kupelekea kupata hasara.
Pia kuokuwa na uhakika wa soko pale mazao yao yanapokuwa tayari.
Nini kifanyike?
- Yafanyike mapinduzi ya teknolojia ya kilimo. Hapa naishauri serekali, wakulima na wadau wa kilimo kufanya mabadiliko katika matumizi ya pembejeo ikiwemo kupunguza au kuachana kabisa na jembe la mkono. Hapa pia inahitajika wakulima wapewe elimu na kuwezeshwa ili waweze kutumia mbegu bora, mbolea, na viuatilifu bora ili kuongeza uzalishaji.
Serekali inatakiwa kuhakikisha kuwa upatikanaji wa mashine za kilimo kama trekta unakua rahisi na kwa bei nafuu. Lakini pia serekali inaweza kuangalia uwezekano wa kununua trekta kwa kila kijiji ili wakulima waweze kulimia hata kwa kukodi lakini kwa bei nafuu. Serekali pia inatakiwa kudhibiti ubora wa mbegu, viuatilifu na mbolea ambazo mkulima anaenda kutumia katika uzalishaji. Pia elimu itolewe kwa wakulima kuhusu teknolojia mpya kama vile matumizi ya “green house, hydroponic”, n.k.
- Kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji ili kuwezesha kilimo kifanyike bila kutegemea mvua. Hapa kwenye miundo mbinu ni pamoja na kuweza kutoa maji sehemu moja kwenda nyingine kwa ajiili ya kilimo mfano; Dodoma sehemu kubwa ina ukame na mikoa jirani ya Iringa na Morogoro ina mito mingi, tunaweza kuangalia uwezekano wa kutumia maji ya mito iliyoko Iringa na Morogoro tukafanyia kilimo Dodoma kwa ku kuchimba mifereji ya maji kutoka kwenye mito hiyo.
Na pia kuhakikisha kwamba wakulima wanakuwa na uelewa wa mbinu za kisasa za umwagiliaji ikiwemo umwagiaji wa matone.
- Kuhakikisha kuwa mkulima anapata soko la mazao yake pindi anapovuna na mkulima aweze kuuza mazo kwa bei nzuri yenye kumpatia faida. Masoko haya yanaweza kuwa ya ndani au nje ya nchi. Masoko ya nje yanapatikana kwa kuimarisha diplomasia na nchi jirani ambazo wana uhitaji wa bidhaa za kilimo kutoka kwetu.
Pia serekali, wakulima na wadau wa kilimo wanapaswa kukaa pamoja na kuunda programu ya simu ambayo itampa nafasi mkulima kuweza kujua masoko ya mazao sehemu tofauti tofauti na bei zake kila siku.
- Kuwekeza kwenye miundombinu ya kusafirishia mazao kutoka shambani kwenda sokoni. Hii ni pamoja na kujenga barabara kwa kiwango cha lami ili barabara zipitike kwa majira yote ya mwaka.
- Kuwatumia wataalamu wa kilimo katika tafiti za kilimo ili kuweza kutatua changamoto za mbegu na magonjwa ambayo yanaathiri mazao ya mkulima. Hapa ni pamoja na kutengeneza mazingira mazuri sehemu za vijijini ili wataalamu hawa wa kilimo waweze kuishi huko karibu na wakulima sio mtaalamu anaishi mjini na mkulima yuko kijijini.
- Bajeti ya kilimo iongezwe ili kukudhi mahitaji ya wizara husika hasa katika kutatua changamoto za wakulima. Sambamba na hilo lazima serekali na wadau wa kilimo wawekeze fedha nyingi kwenye tafiti za kilimo.
- Kuongeza thamani kwenye mazao. Hii ni kuondokana na kuuza mazo ghafi kwa bei ya chini mfano; kama mkulima analima mahindi basi anapaswa kuuza unga na si mahindi vivyo hivyo kwa mazao mengine. Hii itasaidia kuongeza tija kwa mkulima.
Nadhani hayo yote yakifanyika kilimo kitabadilika na uchumi utakua kwa taifa na mtu mmoja mmoja. Na pia itabadilisha dhana ya kuona kilimo kama adhabu na kwamba kilimo ni kwa ajili ya watu masikini tuu.
Mwisho kabisa ifahamike kuwa kilimo ni kazi kama kazi zingine.