Ni vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji. Mahitaji ya maji kwa pilipili hoho huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga maji hupotea kwa urahisi.
MATUNZO YA SHAMBA
Matunzo ya shamba ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu. Matunzo ya shamba hujumuisha;
Soma hapa: sehemu ya kwanza ya kilimo cha pilipili hoho
Umwagiliaji
Njia za umwagiliaji
Kuna njia tofauti za umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya pilipili hoho kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia cane. Kwa kilimo cha kiangazi au pale mvua zinapokuwa hafifu ni muhimu kufanya umwagiliaji wa bustani yako ili kuepuka kunyauka kwa mazao shambani kutokana na upotevu mkubwa wa maji. Wakati wa kumwagilia hakikisha haumwagii maji katika majani bali katika shimo chini ya kichaka cha mche (canopy).
Ratiba ya umwagiliaji
Kwa kipindi cha kiangazi ni muhimu kuwa na ratiba moja ya umwagiliaji wa bustani. Unaweza kumwagilia bustani yako kila baada siku mbili hadi tatu kutegemeana na hali ya hewa na udongo. Cha msingi usiache udongo ukauke bali mwagia maji angalau asilimia hamsini ya unyevu wa udongo unapokuwa umepotea.
maua na matunda ya pilipili hoho
Mambo ya kuzingatia
Ni vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji. Mahitaji ya maji kwa pilipili hoho huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga maji hupotea kwa urahisi. Hakikisha maji hayatuami katika shamba lako kuepuka kuoza kwa mizizi na udongo haukauki.
Kuweka Mbolea
Mbolea ni muhimu sana katika kilimo cha bustani kwa sababu hutoa virutubisho vinavyo hitajika kwa hustawi mzuri wa miche bustanini. Zao la pilipili hoho huitaji sana virutubisho vya Naitrojeni (nitrojen), fosfati (phosphorus), potashi (potassium) na chokaa (calcium). Virutubisho vingine ni pamoja na magnesium, Sulphur, zinc na boron.
Mbolea ya kupandia
Inapendekezwa kutumia mbolea ya kupandia aina ya DAP wakati wa kupandikiza kwa kuweka kiwango cha nusu kizibo cha soda kila shimo au kusambaza kwenye eneo na kuchanganya na udongo wakati wa kuandaa shamba. Mfuko mmoja wa kilo 50 wa DAP unaweza kutosha kutumika katika eneo la ekari moja.
Mbolea ya kukuzia
Weka mbolea ya kukuzia aina ya CAN majuma mawili hadi matatu tangu kupandikiza kwa kiwango cha kizibo kimoja cha soda kuzunguka shina. Mifuko miwili ya kilo 50 inaweza kutumika katika eneo la ekari moja. Vile vile inashauriwa kuweka mbolea ya mchanganyiko (N.P.K.) wakati maua yanapoanza kutoka. Waweza kutumia N.P.K ya maji kunyunyizia majani kila baada ya wiki mbili tangu kutoka kwa maua.
Kupiga Dawa
Dawa za ukungu
Uchaguzi wa dawa za ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika hivyo ni vema kujua magonjwa yanayoshambulia zao la pilipili hoho kabla ya kuchagua dawa za kutumia kama kinga au tiba pale magonjwa yanapojitokeza. Unaweza kuanza kupiga dawa ya ukungu wiki moja tangu kupandikiza au vinginevyo kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.
Dawa za kuua wadudu
Nyinyizia dawa ya kuua wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako ili kuweza kuchagua dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia bustani yako.
Kupalilia
Palizi ifanyike kuanzia wiki ya tatu tangu kupandikiza na kurudia kila baada ya siku 14. Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha kutoka maua na kutengenezwa kwa matunda. Unaweza kupalilia kwa kutumia mikono, jembe dogo la mkono au dawa za viuagugu zinazopatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo. Fuata ushauri wa wataalamu na maelezo ya dawa kama yalivyo kwenye lebo ya chupa.
Kuweka Matandazo
Matandazo husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche. Matandazo ya asili kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema kabla ya kupandikiza baada ya kuandaa matuta.
Kusimikia miti (staking)
Mmea wa pilipili hoho kama ilivyo kwa zao la nyanya huitaji kusimikwa miti ili zisianguke kutokana na mzigo wa matunda na upepo. Simika miti katika bustani ya pilipili hoho wiki tatu tangu kupandikiza hasa baada ya kutoka kwa ua la kwanza. Simika miti yenye urefu wa m 1.5 hadi mita 2 pembeni ya kila mmea umbali wa sm 5 kutoka kwenye usawa wa majani na kufunga kwa kamba shina la mmea na mti kwa kifundo chenye umbo la namba nane. Hakikisha unatumia miti imara isiyooza kwa haraka yenye unene usiopungua sentimita 2.
Kupogolea
Katika mmea wa pilipili hoho upogoleaji hufanyika kwa kundoa majani yaliyo zidi na yaliyo athirika na magonjwa ili kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa katika mmea. Kwa mbegu chotara zinazo zaa kwa muda mrefu pogolea matawi na majani baada ya kuvuna katika kila ngazi ili kuruhusu utengenezwaji mzuri wa matunda kwa ngazi ya juu yake. Vilevile inashauriwa kukata ncha ya shina baada ya kutokea kwa ngazi tano au sita katika mmea ili kuzuia ukuwaji wa mmea kwenda juu na kuchochea ukuwaji mzuri wa matunda. Ondoa ua la kwanza la pilipili hoho kuchochea utokaji wa maua na matunda mengi. Epuka upogoleaji uliokithiri kwani huweza kusababisha hitilafu ya kuungua kwa matunda ya pilipili hoho kutokana na mwanga wa jua.
pilipili hoho tayari kwa kuvuna
KUVUNA
Kiwango cha mavuno
Kiwango cha mavuno ya pilipili hoho kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba. Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno. Kwa wastani mmea mmoja wa mbegu bora (chotara) uliotunzwa vizuri una uwezo wa kutoa karibu kilo 3 mpaka 5 za pilipili hoho.
Muda wa Kuvuna
Pilipili hoho huwa tayari kuvunwa baada ya miezi miwili na nusu hadi mitatu tangu kupandikiza miche. Muda wa kuvuna hutegemeana na matumizi ya pilipili hoho ambapo kwa matumizi ya nyumbani huvunwa zikiwa zimekomaa, ngumu na zenye rangi ya kijani kibichi inayong’aa. Kwa ajili ya kusindika kiwandani huvunwa zikiwa zimekomaa na zenye rangi ya njano au nyekundu kutegemeana na aina ya mbegu iliyotumika. Uvunaji huweza kuendelea kwa muda wa miezi miwili hadi mitatu ukiendelea kuhudumia bustani vizuri. Kwa kilimo cha ndani ya nyumba kitalu (greenhouse) huvunaji huendelea kwa muda wa hadi miezi sita.
Mambo ya kuzingatia
Vilevile usivune pilipili hoho zinazoonyesha dalili ya magonjwa ya kuoza au kuathiriwa na wadudu. Pilipili hoho huvunwa kwa kutumia mikono, kisu au mkasi wa kuvunia. Ni vyema zaidi kutumia kisu au mkasi wakati wa kuvuna kwa sababu shina la pilipili hoho ni laini na hivyo huweza kuathiriwa kirahisi wakati wa kuvuna kwa mikono. Tumia ndoo ya plastiki kama chombo cha kubebea matunda wakati wa kuvuna kwa sababu haipati joto kwa urahisi inapopigwa na jua.
[mc4wp_form id=”665″]
Hatua za uvunaji
Hatua zifuatazo zinaweza kutumika katika uvunaji;
- Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile kisu, mkasi na ndoo ya plastiki kwa kuvisafisha kwa maji safi na sabuni.
- Andaa sehemu utakayokuwa unaweka matunda wakati wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.
- Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha pilipili hoho karibu na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha tunda linabaki na kikonyo chake ili kuzuia maambukizi ya vimelea vinavyoweza kusababisha kuoza kwa pilipili hoho.
- Unaweza kuzamisha kisu au mkasi unaotumia katika kuvuna katika maziwa ya maji kila unapohama kutoka mmea mmoja kwenda mwingine ili kuzuia kueneza ugonjwa wa batobato.
- Ndoo inapojaa matunda beba ukayatandaze katika turubai lililo lilotandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.
- Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya magonjwa.
uvunaji wa pilipili hoho
MATUNZO BAADA YA KUVUNA
Kupakia
Baada ya kuvuna pakia pilipili hoho kwenye matenga au makreti yaliyo tengenezwa kwa mbao au plastiki yenye matundu yanayo pitisha hewa vizuri. Hakikisha upakiaji unafanyika kivulini ili pilipili zisiunguzwe na jua. Pilipili hoho zinapopigwa na jua kwa muda wa masaa mawili hupoteza nusu ya uwezo wake wa kukaa bila kuharibika baada ya kuvuna.
[mc4wp_form id=”665″]
Kuhifadhi
Pilipili hoho huweza kuifadhiwa katika chumba maalum cha kuifadhia (cold room) katika nyuzi joto za sentigredi 7˚C hadi 10˚C na unyevu hewa 95% na kukaa bila kuharibika kwa muda wa wiki tatu hadi tano. Vilevile unaweza kuifadhi pilipili hoho katika chumba chochote kisafi kikubwa chenye nafasi na kisicho na joto jingi chenye madirisha yanayo pitisha hewa vizuri, feni au Air conditioner kwa kupanga makreti au matenga kwa nafasi bila kuyarundika sehemu moja.
Ili kulinda ubora wa pilipili hoho usihifadhi au kusafirisha pilipili hoho pamoja na nyanya zilizoiva au maepo kwa sababu matunda haya huzalisha homoni ya Ethylene inayosababisha kuiva na hivyo kubadilika rangi kwa pilipili hoho. Vilevile hakikisha pilipili hoho zinafika sokoni kabla ya siku tano tangu kuvuna. Ni vizuri zaidi ikiwa zitapelekwa sokoni mara baada ya kuvuna. Cha msingi mkulima anapaswa kuhakikisha soko linakuwa tayari kabla ya kuvuna ili kupunguza adha ya uhifadhi na kukaa muda mrefu na mazao kabla ya kuyauza.