SABABU ZINAZOWEZA KUATHIRI CHANJO
SABABU ZINAZOWEZA KUATHIRI CHANJO KUTOA KINGA KWA KUKU INGAWA WAMECHANJWA : Uzoefu umeonyesha kuwa wafugaji wengi wa kuku wa kisasa(Commercial Chicken) hasa mikoa ya pwani na Dar es salaam, kuku wao hupatwa na magonjwa yaletwayo na virusi licha ya kuwa wamewapa chanjo dhidi ya magonjwa hayo. Tatizo hili limekuwa likitokea hasa kwa ugonjwa wa Gumboro (Infectious Bursal Disease).
Zipo sababu ambazo kama mfugaji hakuzingatia kanuni na taratibu za uchanjaji kuku ugonjwa unaweza kutokea.
SABABU HIZO NI KAMA ZIFUATAVYO:
RATIBA YA CHANJO:
Kutokufuata ratiba ya utoaji chanjo (Vaccination Programme) iliyopendekezwa na mtaalam wa mifugo wa eneo au kanda husika, kunaweza kusababisha kuku wasipate uwezo wa kujikinga na ugonjwa huo ingawa
watakuwa wamechanjwa. Hivyo inashauriwa kufuata ratiba ya utoaji chanjo iliyopendekezwa kitaalam.
Chanjo iliyohifadhiwa katika joto kali hupoteza uwezo wa kufanya kazi. Vilevile kuweka chanjo kwenye freezer huathiri uwezo wa chanjo husika.
Inashauriwa chanjo kuhifadhiwa kwenye hali ya ubaridi wa joto kati ya nyuzijoto 2oC-8oC hasa kwenye friji.
UGONJWA:
Iwapo kuku tayari wameshapata virusi vya ugonjwa husika, wanaweza wakaugua ugonjwa huo hata kama watachanjwa chanjo ya ugonjwa huo.
KUTOFUATA MASHARTI YA WATENGENEZAJI WA CHANJO KUHUSU MATUMIZI YA CHANJO:
(Manufacture’s instructions) Kuhusu matumizi ya chanjo ambayo hutolewa na wataalamu wa mifugo au wauza madawa ya mifugo wanaotambulika katika kutoa huduma hiyo. Hivyo ni muhimu kuzingatia masharti ya mtengenezaji chanjo husika.
USAFIRISHAJI NA UTOAJI CHANJO:
Usafirishaji wa chanjo katika mazingira yasiyofaa huathiri nguvu ya chanjo, pia
utoaji wa chanjo yenyewe na wataalam wa mifugo au madawa ya mifugo huathiri zoezi lote (Vaccination procedure) la uchanjaji wa kuku. Inashauriwa chanjo isafirishwe kwenye chombo au kifaa chenye ubaridi au chenye uwezo wa kuhifadhi joto linalotakiwa, pia kuzingatia taratibu zote za mwenendo wa kuchanja kuku.
LISHE DUNI:
Chakula ambacho kina viinilishe duni vinavyohitajika kukidhi afya bora ya kuku husababisha kuku kuwa dhaifu, hivyo huwa mwili wa kuku hauna uwezo wa kijikinga na magonjwa. Hivyo ni vema kulisha chakula cha kuku chenye ubora unaokidhi mahitaji ya afya ya kuku.
UTUMIAJI WA DAWA ZA TIBA NA CHANJO KWA PAMOJA:
Hii pia huathiri uwezo wa chanjo kufanya kazi kwenye mwili wa kuku. Ni vema kutowapa chanjo na dawa za tiba (antibiotics) kwa wakati mmoja. Inashauriwa kutowatibu kuku siku mbili kabla na baada ya chanjo kutolewa pia wapewe vitamini kama vitalyte, Poultry antistress, vitastress, stressvita n.k.
VIJISUMU (MYCOTOXINS):
Hivi ni vijisumu ambavyo huwa kwenye chakula cha kuku kilichohifadhiwa vibaya kama vile unyevunyevu au kwenye tandiko (litter materials) chafu, hivyo kuku akila chakula chenye vijisumu hivi hupunguza kinga za mwili kupambana na magonjwa, kwani vijisumu hivi hushambulia sehemu muhimu ndani ya mwili wa kuku ambazo hujihusisha na kinga na magonjwa. Hivyo inashauriwa vyakula vya kuku vihifadhiwe kwenye sehemu isiyokuwa na unyevunyevu au joto kali, pia nafaka zinazotumika kutengenezea chakula ziwe zimekauka vizuri. Upatapo chakula cha kuku changanya na vitu vinavyosaidia kupambana na vijisumu hivi. Waweza kutumia Farmacid premix na mycobind kwenye chakula.
USUMBUFU (STRESS):
Kuku waliopata usumbufu siku chache kabla au baada ya chanjo huwa wanapungukiwa uwezo wa kupokea chanjo ili kujikinga na ugonjwa, usumbufu unaweza kuwa msongamano(Overstocking) kukata midomo(beak trimming), kuwahamisha kuku kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hivyo epuka usumbufu kwa kuku unapokaribia muda wa kuwapa chanjo kuku ili kufanya chanjo ifanye kazi vizuri.