Ubebeshaji miche ya mikorosho ni moja ya mbinu muhimu katika uendelezaji wa zao la korosho kwa sababu ni teknolojia pekee inayohakikisha usahihi wa viwango vya uzalishaji wa aina ya mkorosho uliopandwa.
Kwa kutumia mbegu, huwezi kuwa na uhakika na uzalishaji wa aina ya mbegu ulioitumia kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa mbegu kubadilika tabia na kuwa tofauti na tabia ya mti mama.
Teknolojia ya ubebeshaji inamwezesha mkulima kutabiri mavuno na ubora wa korosho shambani mwake kama ukubwa wa korosho, sura yake, rangi, uzito na sifa zingine kulingana na mti mama.
Faida za ubebeshaji ni pamoja na
• Miche ina nguvu ya kutosha kuhimili mazingira.
• Ni rahisi kustawi katika mazingira mbalimbali.
• Mmea uliobebeshwa una tabia sawa na mti mama.
Mapungufu ya ubebeshaji
• Unaweza kueneza tabia mbaya ya aina moja ya mikorosho.
• Ni vigumu kuzalisha na kusambaza idadi kubwa ya miche iliyobebeshwa kwa wakati mmoja ukilinganisha na mbegu.
Jinsi ya kuanzisha Kitalu na kukitunza.
Mkulima anashauriwa kuanzisha kitalu kulingana na mahitaji yake na ambacho anaweza kukihudumia vizuri. Uzoefu unaonyesha kwamba kitalu kinahitaji uangalifu mkubwa katika hatua zote za kuchagua eneo, kuatika mbegu, kuchagua vikonyo na kubebesha na matunzo ya kitalu.
Mahitaji na Vifaa vinavyohitajika kabla ya kuanzisha kitalu.
Kabla hujaanza kubebesha nimuhimukwanza uandae kitalu ambacho unaweza kupunguza ama kuongeza mwanga, viriba, nailoni nyeupe ya kubebeshea, maji ya kutosha, mbolea ya samadi, mbegu, mikorosho ya kuchukua vikonyo, ndoo ya kumwagilia maji, sepetu, kisu kikali cha kubebeshea, majembe, toroli na vinginevyo.
Kuchagua eneo linalofaa kwa kitalu.
Mambo muhimu ya kuyazingatia wakati wa kuchagua eneo linalofaa kuanzisha kitalu cha miche iliyobebeshwa ni pamoja na :
• Eneo la kitalu liwe sehemu tambarare na isiyotuamisha maji kwani maji mengi kwenye kitalu yanaweza kusababisha kuoza kwa miche.
• Kitalu kiwe karibu na chanzo cha maji yasiyo na chumvi chumvi na yanaweza kupatikana muda wote.
• Kiwe karibu na makazi na kisiwe mbali sana shamba lililokusudiwa.
• Kibiashara, kitalu kiwe karibu na wateja wa miche.
Ubebeshaji
Ubebeshaji nikitendo cha kuunganisha miti mawili pamoja ili kupata mti mmoja. Ubebeshaji ni kitendo cha kuunganisha kishina mama na kitawi shina kwa madhumuni ya kupata mche mmoja wenye sifa unazozitaka. Hivyo, madhumuni ya kubebesha mikorosho ni:
• Kuunganisha miti mawili ya mikorosho yenye sifa tofauti kama kishina cha mkorosho mfupi na kitawi shina cha mkorosho wenye sifa ya kuzaa sana, ukubwa wa korosho, kustahamili mashambulizi ya wadudu na magonjwa nk
• Kupunguza muda wa kuzaa tokamiaka 3 hadi 5 ya mikorosho iliyopandwa kwa kutumia mbegu hadi mwaka mmoja tu toka kupanda hadi kuvuna.
• Kuwezesha kubadilisha mti wa mkorosho wenye sifa mbaya kwa kukata shina lake na kubebesha vitawi shina toka kwenye mkorosho wenye sifa unazotaka juu ya machipukizi yatakayojitokeza..
Sifa za Kishina Mama
Kishina mama kinachofaa kubebeshwa kiwe na sifa muhimuzifuatazo:
• Kiwe na unyevu wa kutosha ili kupata mmea wenye afya mzuri
• Kiwe na ukubwa unaofanana na kitawishina
• Kisiwe kimeshambuliwa na wadudu na magonjwa.
Sifa za Kitawi shina
• Kisiwe kimenyauka
• Kitokane na mkorosho wenye sifa unazozitaka kama kuzaa sana, kustahamili mashambulizi ya magonjwa na wadudu, ukubwa wa korosho nk
• Kiwe kimekomaa na ukubwa sawa na shina mama.
Jinsi ya kuandaa shina mama na kitawi shina
Mafanikio katika ubebeshaji yanatemea sana ubora wa kitawi shina. Ni muhimu kuhakikisha kwamba unapata kitawi shina toka kwenye mkorosho ambao haujashambuliwa na wadudu na magonjwa na kiwe katika hali mzuri, yaani kisiwe michubuko na machipukizi yanayoendelea kukua.
Hivyo inapendekezwa kuvuna kitawi shina kwa kuzingatia yafuatayo:
• Inashauriwa kuvuna kitawi shina wakati wa ubaridi kama mapema asubuhi
• Chagua kishina chenye ukubwa unaofanana na vishina mama vyako. Tumia kisu kikali wakati wa kukata.
• Weka alama kwenye vitawi shina vyako ili baadae uweze kufahamu aina ya mkorosho uliobebesha
• Virigia vitawi shina vyako kwenye gazeti lililoweshwa maji na kuvihifadhi kwenye chombo chenye ubaridi.
Hatua za ubebeshaji
• Chonga pande mbili za kitako cha kitawi shina kiasi cha urefu wa sentimita mbili na nusu ili upate umbo la kabari.
• Kata kishina juu ya majani mawili kwa kutumia kisu kikali. Pasua katikati kiasi cha sentimita mbili na nusu kuelekea chini
• Pachika kitawi kwenye nafasi ya kishina iliyopasuliwa. Oanisha magamba ya kitawi na kishina yawe sambamba.
• Funga ungio la kishina na kitawi kwa kutumia utepe wa nailoni wenye upana wa sentimita moja. Kaza utepe huu kwani kazi yake kubwa ni kuzibana sehemu zilizokatwa za kishina na kitawi mithili ya kidonda cha binadamu kinachoshonwa ili nyama ziungane.
• Zungushia utepe wa nailoni ungio pamoja na kitawi kizima .Kazi ya utepe huu wa pili ni kuhifadhi maji ya kitawi kisanyauke. Umande utakaojitokeza ndani ya utepe huu ni ishara kwamba kitawi hakinyauki
• Weak miche yako kwenye kivuli na ipangwe kwenye mistari. Mwagilia maji mara baada ya kubebesha na endelea kumwagilia maji mara moja kwa siku. Chunguza dalili za kuchipuza vitawi kuanziawiki ya pili toka kubebesha huku ukiondoa machipukizi yote yanaoota chini au kwenye ungio.
• Lege\za utepe wa pili mara unapooona dalili za kuchipua ili kuruhusu majani yaote.
• Ukiona dalili za utepe wa kwenye ungio unabana, ulegeze ama ondoa. Miche yako itakuwa tayari kwa kupeleka shamani na kuipandikiza baada kuota majani manne au zaidi yaliyokomaa.
• Punguza kivuli kwenye kitalu taratibu na hatimae ondoa kabisa ili miti iweze kuzoea mazingira ya shambani siku cha kabla ya kuipeleka shambani.
UBEBESHAJI WA MITI MIKUBWA – TOP WORKING
Top working ni kitendo chakubebesha miti ya mikorosho mikubwa. Madhumuni ya kubebesha miti mikubwa ni
• Mikorosho mikubwa, hasa ile iliyopandwa kwa kutumia mbegu kubadilika tabia kinyume na matarajio kama, kushambuliwa na wadudu na magonjwa ama kutozaa vizuri.
• Mabaliko ya matakwa ya masokokama kupendelea korosho kubwa badala ya ndogo
• Kuzuka kwa magonjwa hatari mapya
• Kugunduliwa ama kutolewa aina mpya ya mikorosho ambayo ni bora zaidi, hivyo mkulima kuhitaji kuibadilisha bila kupanda upya.
Faida ya kubebesha mikorosho mikubwa
• Kuboresha mikorosho isiyozaa pasipo kuanza kulima sham,ba jipya.
• Kuirudishia mikorosho isiyozaa katika hali uzalishaji kwa muda mfupi.
• Huharakisha uzalishaji wa vitawi shina kwa usambazaji kwa wakulima
Hatua za ubebeshaji mikorosho mikubwa
• Hatua ya kwanza ni kukata shina la mti wa mkorosho unaokusudia kufanya top work kwa kuzngatia umri wa mkorosho, kimo cha kukata ,muda wa kukata na kukata kwa utaratibu usiioleta mshindo mkubwa wakati wa kuunguka.
• Kupaka mta na kufunika kwa majani juu ya shina lililokwa
• Baada ya machipukizi kufikia ukubwa wa penseli,hatua inayofaa ni kuundaa vifaa muhimu kama ilivyo kwa ubebeshaji wa kwenye vishina yaani kisu kikali na nailoni
• Chagua machipukizi yanayokaribia mkato na kuikata minginn yote ambayo haihitajiki
• Bebesha kwa kufuata utaratibu wa ubebeshaji kama ilivyo kwa vishina mama.
Matunzo ya miti mikubwa iliyobebeshwa:
Baada ya kukamilisha ubebeshaji, miti mikubwa inahita huduma maalum. Kwa kawaida machipukizi yaliyobebeshwa kwenye miti mikubwa yanakua haraka haraka sana. Dalili ya kufanikiwa kwa machipukizi yaliyobebeshwa ni kuata machipukizi chini ya maungio. Baadhi ya mambo muhimu ya kuyazingatia ni pamoja na:
• Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuondoa maotea mengine yanayoota kwenye chipukizi chini ya maungio
• Majani yakijitokeza na kukua, ondoa nailoniya kwenye maungio
• Fungia chipukizi lililobeshwa na nguzo ya mti ili kuzuia lisiangushwe na upepo. Fungia kwa kamba aina ya kudu kwa kifundo chenye umbile na nane
• Punguza matawi yanayoota kwenye machipukizi yaliyobebeshwa ili yakue vizuri.
• Kagua shina zima kwa makini ili kudhibiti mashambulizi ya kifauongo
• Baada ya mwaka mmoja, ondoa machipukizi dhaifu yote na kuyaacha manne tu yenye nguvu na ustawi unaoridhisha.
• Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa kwanza mti mkubwa wa mkorosho uliobebeshwa unahitaji matunzo yote muhimu katika kama ilivyoelekezwa katika kanuni ya kilimobora cha zao la korosho.