
UBUYU TUNDA LENYE FAIDA KUBWA MWILINI : Mbuyu, Adansonia digitata jina la kitaalaam lililopewa mti huu kwa heshima ya mtafiti mvumbuzi Michael Adanson, aliyefanya utafiti kuanzia kati ya miaka ya 1700, uliutaja kuwa ni‘’ mti mkubwa wenye matumizi ya ajabu’’. Mbuyu unaweza kufi kia urefu wa mita 20 na kigogo chake kinaweka kiasi kikubwa cha maji kinachoufanya mti huu huvumilia kipindi kirefu cha ukame na unaweza kuishi kwa miaka 500. Jina la kiingereza la “baobab” linatokana na tunda lake kuwa na mbegu nyingi kitu ambacho awali waarabu walikitaja kuwa “bu-hibab” lenye mbegu nyingi.
Ubuyu ni tunda linachukuliwa na watu wengi kama tunda lisilokuwa na thamani yeyote. Pengine ni kwa sababu hutumiwa zaidi na watoto au watu wa hali ya chini kiuchumi. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi, ubuyu una kiwango kikubwa cha vitamin C hata kuyazidi matunda mengine kama chungwa. Imegundulika kwamba kiasi cha gramu 100 za ubuyu ina miligramu 300 za vitamini C, kiasi mara sita zaidi ya kiasi kile kinachopatikana kwenye tunda kama tunda ambalo ndilo linaloaminika kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini C.
Kama inavyojulikana vitamini C ni muhimu sana mwilini, kwani ndiyo inayotukinga dhidi ya magonjwa nyemelezi. Ndiyo maana hapa nchini imekuwa ikisisitizwa na wataalamu wa lishe kuwa wagonjwa wenye upungufu wa kinga mwilini au wenye virusi vinavyosababisha ukimwi, watumie sana ubuyu ili kuongeza kinga mwilini.

Hii inatokana na ukweli kwamba ubuyu una virutubisho vingi vya kukinga mwili, Vilevile wataalamu wa lishe wamethibitisha kuwepo kwa vitamini B2 ambayo huimarisha ukuaji wa nyama, ngozi, na kuongeza nuru ya macho. Hali kadhalika, kuna vitamini B3 ambayo ni muhimu kwa uimarishaji wa mchakato wa umeng’enywaji wa chakula mwilini.
Mbali na vitamini, tunda hili lina madini mafuta (fatty acids) kiasi cha gramu 100, miligramu 2.93 za madini aina ya kalisi, miligramu 2.31 za potassium, na miligramu 118 za fosiforasi. Hii inadhihirisha umuhimu wa ubuyu kutokana nakusheheni vitamini na madini.

Aidha ubuyu pia unatibu pia ugonjwa wa kuharisha mababu zetu walitumia sana kudhibiti maradhi ya kuhara hata kipindupindu.
Kwa mujibu wa habari za hivi karibuni biashara ya ubuyu inazidi kuongezeka barani Afrika, hususani Tanzania kwenye mikoa kame na sehemu za mijini.
Hitimisho:
Kwa ujumla ubuyu si tunda la kudharau kama ambavyo baadhi ya watu hujaribu kuonesha, anza sasa kupenda matumizi ya ubuyu kwa faida ya afya yako, kwani utafiti umeshatibitisha zao hili lina virutubisho vingi na muhimu kwa afya ya binaadamu. Kwa kutambua kuongezeka umuhimu wa zao hili hivi karibuni serikali yetu imeipa kipaumbele uzalishaji, utunzaji na soko la zao hili kwa kuelekeza majukumu kwenye wizara tatu. Jukumu la utunzaji limewekwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, uzalishaji upo chini ya Wizara ya kilimo na Chakula wakati soko lake linasimamiwa na wizara ya Viwanda na Biashara.