UFUGAJI BORA WA SUNGURA KIBIASHARA


UTANGULIZI.

Kabla hujaamua kufuga sungura hakikisha ya kwamba umejitoa na una muda wa kuwahudumia wanyama waha, ufugaji wao si rahisi kama vile ukifuga paka au mbwa, sungura wanahitaji uangalizi na hassa kwenye usafi kwa sababu ni rahisi kwao kupata maradhi yatokanayo na mazingira mabaya na machafu.

Ikiwa mfugaji anataka kunufaika na sungura anaowafuga basi ni sharti ahakikishe wana afya njema, kwani hii ndiyo changamoto mojawapo kwa ufugaji wa sungura, magonjwa ya sungura hasa huwa ni ya tumbo na kifua.

Tatizo hasa ni kwamba, wataalamu bado hawajagundua dawa maalumu za magonjwa ya sungura kwa hivyo ni muhimu kwa mfugaji kuhakikisha sungura wake hawapatwi na magonjwa. Sungura aliye na afya ni yule ambaye ngozi yake ni nyororo, macho mazuri yasiyo na kasoro, asiye na vidonda vya ngozi, katika macho, midomo, au kwenye masikio.

Uchafu kwenye miguu na pua ni ishara ya ugonjwa wa kukohoa kwani sungura huosha pua zake kwa kutumia miguu ya mbele. Pia unaweza kumuweka chini na kutazama dalili za ugonjwa anaporuka.

FAIDA ZA KUFUGA SUNGURA.

(i) Ufugaji wa sungura unaweza kuongeza pato la familia wakati ukiendelea na majukumu mengine. Unaweza kuwauza kwa watu binafsi, wasindikaji wa nyama, wafugaji wa nyoka, maduka ya wanyama wa mapambo, bustani za wanyama na kadhalika. Pia inaweza kuwa ni utashi mzuri wa kujenga uhusiano wa karibu na wanafamilia kwa sababu daima mtakuwa mkishiriki kwenye shughuli za utunzaji.

(ii) Unaweza kuzalishaji lishe yako mwenyewe na nyama ya kutosha, kwani nyama ya sungura inafahamika kwamba ina lishe bora sana kwa binadamu. Utaokoa fedha zako za ununuaji wa kitoweo, kwani hutaweza kununua nyama nyingine kwa bei ya juu wakati unaweza kuchinja sungura wako na kujipatia hadi kilo nne za nyama kwa familia.

(iii)    Sungura wanahitaji sehemu ndogo ya kuwafugia kuliko wanyama wengine. Hili ni jambo muhimu, hususan katika maeneo ambayo hayana ardhi ya kutosha ya kilimo, hasa mijini. Sungura, kwa wafugaji wadogo, wanaweza kufugwa katika mabanda ya ndani; kama maeneo ya gereji au vyumba vya ziada. Kwa wafugaji wa kati wanaotaka kuwa na kundi kubwa la sungura kibiashara, wanaweza kuhitaji eneo dogo lisilofikia hata ekari moja, kwani ni eneo dogo tu linalohitajika kujenga mabanda.

(iv) Kuhusu suala la kazi, ufugaji wa sungura hautumii nguvu nyingi kama ilivyo kwa shughuli nyingine za kilimo. Inakadiriwa kwamba unatakiwa kutumia wastani was aa 14 hadi 20 kwa mwaka kumhudumia sungura jike mmoja na saa 14 hadi 20 kwa wiki kuwahudumia sungura majike wanaozaa 100.

(v) Pato la ziada linaweza kupatikana kwa kuuza sungura hai kwa wafugaji wengine au kwa kuzalisha na kuua minyoo kutokana na kinyesi cha sungura, ambacho pia unaweza kukiuza kwa ajili ya mbolea.

(vi) Mkojo wa sungura ni dili kubwa viwandani, hivyo ukijifunza namna ya kuukusanya unaweza kuingiza fedha nyingi huku ukiendelea na shughuli nyingine.

HASARA ZA KUFUGA SUNGURA
Kila kitu duniani kina faida na hasra pia sungura na ufugaji wake unahasara kadhaaa japo sio kubwa kama za biashara nyingineyo.

(i) Uwekezaji wa awali ndiyo gharama kwa sababu ya kununua sungura wa kuanzia pamoja na kujenga banda na kununua vifaa vinavyotakiwa. Gharama hizi, hata hivyo, zinaweza kupungua ikiwa utatumia banda ama eneo lililopo, au kama utaamua kujenga banda la kawaida kulingana na rasirimali zilizopo badala ya kuingia kwenye ujenzi wa mabanda ya kisasa ambayo gharama zake ni kubwa zaidi.

(ii) Biashara ya ufugaji wa sungura siyo maarufu sana ikilinganishwa na shughuli nyingine za kilimo; kwa maana hiyo wengi huichukulia kama ni biashara isiyotabirika na yenye gharama. Ni muhimu kuwa na upeo kidogo wa masoko kabla ya kuanzisha biashara hiyo.

PITIA
Umuhimu wa kitunguu swaumu katika kutibu magonjwa ya kuku

Hata hivyo, kwa kuwa hivi sasa serikali inahimiza shughuli za kilimo na ufugaji ambazo zina ubunifu, ni wazi kwamba hata biashara ya sungura itapatiwa ufumbuzi mkubwa, kwani tayari kuna wafugaji kadhaa nchini. Muhimu tu ni kuunda umoja unaoweza kutumika pia kutafuta masoko ya uhakika.

(iii)   Mfugaji anayeanza biashara hiyo anaweza kukabiliana na changamoto za utunzaji na hawezi kuona uzalishaji mkubwa kwa miaka miwili ya kwanza. Hii ndiyo sababu ufugaji wa sungura unajulikana kama “Biashara ya miezi 18”, kwa kuwa wafugaji wengi huamua kuachana nayo hata kabla hawajamaliza mwaka wa pili.

(iv)      Japokuwa unatumia saa chache, lakini ufugaji wa sungura ni biashara ya kila siku kwa sababu wanahitaji kulishwa na kunyweshwa kila siku. Kwa kuwa mwanzoni faida yake siyo kubwa, ni vigumu kutafuta mfanyakazi.

ZIADA
Wafugaji wengi wa sungura vijijini na mijini wanawafuga kama mapambo, lakini hawaelewi kwamba wanyama hao wadogo wanaweza kuwapatia mapato makubwa ikiwa watawafuga kibiashara.

Nyama ya sungura ni nzuri sana, na kama itakaangwa ama kupikwa vizuri unaweza usijue kama ni ya kuku ama mnyama gani.

Ufugaji wa sungura umekuwa ukiwaletea tija wajasiriamali wengi katika baadhi ya mataifa, na nchini Tanzania ujasiriamali huu umeanza kushika kasi sana hasa katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako nimepata kushuhudia vijana na watu wazima wanaojihusisha na ufugaji huo wakishiriki hata kwenye maonyesho ya kilimo (Nane Nane).

Huu ni ufugaji endelevu, wenye kutunza mazingira ambao mbali ya kukupatia chakula mezani na kipato bila kutumia mtaji mkubwa, lakini utabadili uchumi wa familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Faida zake ziko nyingi sana: Unaweza kuuza mkojo wa sungura kwa ajili ya matumizi ya maabara, kinyesi chake ni mbolea nzuri au unaweza kukitumia kuzalisha minyoo ambayo ni chakula bora cha kuku wa kienyeji, na nyama yake ni tamu sana. Kuna wengine wanasema miguu yake inaleta bahati, lakini siwezi kuwadanganya kwa sababu ninaamini tu katika Mungu.

Unachotakiwa kukifanya ni kuandaa mpango wako mdogo kuhusu namna ya kuanza bila kutumia gharama kubwa sana, kama wanavyoelekeza wataalamu wengi.

Huhitaji kuwa na mamilioni ya fedha kuanzisha ufugaji wa sungura, bali unaweza kuanza na mtaji mdogo kwa kutumia rasilimali zilizopo na ukafanikiwa.

Kwa kutumia uzoefu wangu wa ufugaji, nitajitahidi kueleza kwa hatua ili uweze kuepuka changamoto. Si mnafahamu kwamba kila biashara ina changamoto zake? Unapaswa kukabiliana nazo.

Lakini kumbuka kwamba, uzoefu ni mwalimu mzuri zaidi kuliko kusoma tu kwenye vitabu. Unaweza kuwatembelea watu wanaofuga sungura na ukajifunza kwa undani wanafanyaje hata kabla ya kuanzisha biashara yako ya kuwafuga.

Uzuri wa ufugaji wa sungura ni kwamba, unaweza kuwafuga hata hapo mjini unapoishi endapo utawatengenezea banda maalum. Siyo tu kwamba hawahitaji uangalizi wa saa 24, lakini pia wanatoa nyama ya kutosha na faida nyingine ambazo nitazieleza kwa kina katika makala zijazo.

Jambo la muhimu la kulielewa ni kwamba, ukizingatia matunzo mazuri na kuwapatia mazingira bora, ndani ya mwaka mmoja unaweza kuwa na kundi kubwa la sungura kutoka sungura wako majike wawili tu na dume moja.

Najua faida ya mifugo kwa sababu nimezaliwa na kukulia katika mazingira ya ufugaji ingawa wakati huo hakukuwa na maendeleo kama ya sasa.

Leo hii ninapozungumzia fugaji wa sungura natambua kwamba uwekezaji huo unaweza kukuletea tija katika njia nyingi tu kama kuuza mkojo wa sungura kwenye maabara mbalimbali, kupata samadi kutokana na kinyesi chao ambacho pia hutumika kuzalishia mionyoo. Nyama, hata hivyo, ndiyo bidhaa kubwa na muhimu.

PITIA
Ufugaji wa nyuki kwa njia ya kisasa

Ninachotaka kuwaelekeza hapa wajasiriamali wenzangu ni kitu rahisi tu katika uanzishaji wa ufugaji wa sungura kwa kuanzia na kile ulichonacho, siyo kama wanavyoelekeza wale wanaoitwa wataalamu.

Tunafahamu hali zetu za uchumi zilivyo, hivyo tukianza kuwaza kuhusu mtaji mkubwa kamwe hatuwezi kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

Kwa maana hiyo, tunapaswa kuanza katika mazingira tuliyopo, kwa rasilimali zilizopo na tunaweza kukua taratibu hadi kufikia kwenye uwekezaji mkubwa katika ufugaji wa sungura.

MAMBO YA MSINGI
Kuna mambo mengi ambayo unapaswa kuyafahamu kabla ya kuanza ufugaji wa sungura. Lakini nitajaribu kueleza kwa nia ya kukupa mwangaza wa namna ya kuanzisha ufugaji huo. Kadiri unavyoendelea, na ikiwezekana, unatakiwa kupata taarifa za kutosha kuhusu ufugaji huo, kuanzia ujenzi wa mabanda, jinsi ya kuwahudumia, uchunaji wake baada ya kuwachinja, kuweka kumbukumbu na kadhalika.

Binafsi naweza kutumia dakika tano tu kumchuna sungura, tofauti na unavyotumia muda mrefu kunyonyoa kuku. Sungura hawana msimu wa kuwafuga, unaweza kuanza ufugaji wakati wowote na wanaweza kuanza kuzaliana wakati wowote, tofauti na wanyama wengine.

Sungura majike wawili na dume moja wanaweza kukupatia wewe na familia yako kiasi cha kilogramu 81 za nyama kwa mwaka, kiasi ambacho ni kingi kwa familia za wastani wa watu watano.

MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA SHUGHULI YA UFUGAJI WA SUNGURA. TABIA ZA SUNGURA WAKO

Kitaalam mtu yeyote anaepanga kuanzisha mradi wa ufugaji wa sungura anatakiwa kuwa makini na mambo yafuatayo;
1. Aina ya sungura. Kufahamu aina ya sungura anayotaka kufuga na yenye kuendana na mazingira anayoishi maana kuna aina nyingi za sungura wafugwao duniani.

2. Hali ya hewa ya eneo unalotaka kufugia. Hapa tunaangalia zaidi katika unyevunyevu na joto katika eneo husika. Hivyo sehemu nzuri kwa ajili ya kuzalishia sungura ni sehemu yenye joto la wastani 26oC-27oC ambayo itawafanya wakue kwa afya njema

3. Suala la lishe linachukua asilimia 70-80 katika ukuaji wa sungura Hivyo ulishaji wa chakula bora kwa sungura huleta mabadiliko makubwa katika ukuaji wao na lishe mbaya huwafanya kutokuwa na afya bora na ukuaji wao huzorota.Sungura hupendelea zaidi majani na chakula cha kuchanganya kwa kuzingatia mahitaji yao.

4.Magonjwa Kama walivyo wanyama wengine sungura nao hushambuliwa na magonjwa pamoja na viroboto ambayo husababisha kuzorota kwa ukuaji wa sungura na inaweza kusababisha hadi kifo. Mfano wa magonjwa ambayo mara kwa mara huwasumbua sungura ni koksidiosis, “enteritis” na “pasteurellosis”

5. Ufahamu juu ya ufugaji wa sungura. Ufugaji wa sungura una taratibu zake na zinatakiwa kufuatwa ili kuw ana matokeo bora katika shughuli yote ya ufugaji wa sungura.

Hivyo mfugaji anatakiwa kufahamu mbinu zote kuanzia anapomleta sungura bandani mpaka anapoenda kumuuza. Ni matumaini yangu kuwa wewe mfugaji mtarajiwa hata wewe ambaye tayari umeshaanza kufuga umeweza kufaidika na kujifunza mbinu muhimu unazopaswa kuzitambua kabla ya kuanza mradi wa kufuga sungura, ukiweza kuzizingatia mbinu hizo utaweza kujikomboa wewe na familia yako lakini pia utawakomboa watanzania katika suala la ajira.

AINA ZA SUNGURA WA KUFUGWA
Kwa kawaida, mfugaji anahitaji kutambua sungura ambao atatumia kama mbegu kwa kuzalisha wengine wenye ubora wa hali ya juu. Ni vyema kutenga sungura wangali wadogo wakiwa miezi minne kwa wa kike na miezi sita kwa sungura wa kiume, yaani kabla hawajaanza kuzaa.

Baada ya kupandisha kwa mara ya kwanza na wanapopata mimba sungura hao wa kike ni vyema kuwatenga na kuwaweka katika chumba chao maalum ili kuanzisha kizazi kingine.

PITIA
Kilimo Bora Cha Bilinganya

Kuna aina mbali mbali wa sungura lakini wanagawanywa mara mbili kwa matumizi. Moja ni kwa matumizi ya ngozi yake kwa kutengeneza kofia, mifuko, na mishipi na pili kuna aina ya sungura ambao hufugwa kwa kuzalisha nyama.

KUCHAGUA AINA YA SUNGURA
Kama nilivyosema awali, kabla ya kuanza biashara ya ufugaji wa sungura unapaswa kuamua ni aina gani ya sungura unaotaka kuwafuga. Aina mbili zinazopendwa zaidi na wafugaji kwa ajili ya nyama ni New Zealand White na California White ambao wana nyama iliyo bora zaidi.

KUCHAGUA AINA YA SUNGURA
Kama nilivyosema awali, kabla ya kuanza biashara ya ufugaji wa sungura unapaswa kuamua ni aina gani ya sungura unaotaka kuwafuga. Aina mbili zinazopendwa zaidi na wafugaji kwa ajili ya nyama ni New Zealand White na California White ambao wana nyama iliyo bora zaidi.

AINA KUMI 10 BORA ZA SUNGURA WA NYAMA.

1) NEW ZEALAND WHITES: Hii ni jamii mojawapo maarufu kwa ufugaji wa sungura wa nyama, na kwa nchi kama Marekani, nyama yake ndiyo bora zaidi kuliko aina nyingine za sungura. Sungura hawa wanaweza kufikisha kilogramu 3.6 hadi 5.

2) CALIFORNIAN WHITE RABBITS: Hawa ni uzao chotara wa sungura jamii ya Chinchilla na New Zealand Whites. Wana manyoya meupe na madoa meusi na wanafahamika kutokana na maumbile yao kama matofali na wanatoa nyama nzuri. Wanaweza kufikisha kilogramu kati ya 3.2 hadi 4.8.

3) AMERICAN CHINCHILLA: Hawa ni aina bora ya sungura kwa ajili ya nyama na wanarandana na sungura jamii ya Chinchilla ambao hata hivyo ni wakubwa kwa maumbo. Wana rangi ya kijivu na nyama yao inaweza kufikisha hadi kilogramu 3.6. Nyama yake inapendelewa Zaidi kukaangwa ama kubanikwa.

4) SILVER FOXES: Hawa ni sungura rafiki zaidi kufugwa majumbani ambao wanafaa kwa mapambo pamoja na nyama. Aina hii ni adimu sana na wanaweza kufikisha kilogramu kati ya 4 hadi 5. Wana rangi ya fedha yenye kivuli cheusi na masikio yeliyoinuka, kama alivyo mbweha wa rangi ya fedha.

5) CHAMPAGNE D ARGENT: Aina hii ya sungura wa kihistoria anayevutia imetumiwa kwa nyama tangu mwaka 1631. Nyama yao inapendwa ulimwenguni kote na ni wazuri kwa kufugwa. Unaweza kuwakuta katika rangi mbalimbali kama nyeupe, rangi ya maziwa au chocolate.

6) CINNAMONS: Hawa ni uzao chotara kati ya sungura wa New Zealand White na American Chinchilla. Maumbile yao yamerandana na asili yao. Sungura hawa wanatoa nyama nzuri na wanafugwa zaidi kibiashara kwa ajili ya nyama.

7) SATINS: Hawa ni sungura wakubwa na wazito ambao wanatoa kiwango kikubwa cha nyama. Ni wazuri kwa kufugwa kwa ajili ya nyama. Maumbile yao ni ya kati na wanapatikana katika rangi mbalimbali kama bluu, nyeusi, shaba, chocolate, nyekundu, Siame na otta.

8) Rex: Sungura hawa wenye manyoya laini yanayoteleza hufugwa kwa ajili ya manyoya na nyama. Wanapokuwa wakubwa wanaweza kufikisha kati ya kilogramu 3.2 hadi 4. Wana rangi za bluu, amber na madoa meupe. Nyama yao ni nzuri na wanafaa sana kufugwa.

9) PALOMINO: Hawa ni jamii bora ya nyama na wanafugwa kibiashara kwa ajili ya nyama tu. Ni wapole na wanafaa kufugwa nyumbani. Wanaweza kufikisha kati ya kilogramu 3.2 hadi 4.5.

10) FLEMISH GIANTS: Kama lilivyo jina lenyewe, sungura hawa ni wakubwa kwa umbo na wanaweza kufikisha kilogramu 10. Wana miili mikubwa na mipana na kwa maumbile haya pia wanakula sana. Ni wazuri kufugwa kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

KILIMO BORA CHA UFUTA

Ufuta (sesamum indicum)ni zao linalolimwa kwa wingi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga na ukanda wa chini katika mikoa ya Rukwa

Read More »

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »