UFUGAJI WA KISASA WA NG’OMBE

UTANGULIZI
Ng’ombe wanafugwa kwa ajili ya nyama na maziwa lakini pia hutoa mazao mengine kama ngozi,mbolea na hutumika kama wangyama kazi.  Zaidi ya asilimia95 ya ng,ombe na hutumika kama wanyama kazi.  Zaidi ya asilimia 95 ya ng’ombe wanaofugwa hapa nchini ni wa asili ambao huzalisha nyama na maziwa kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na wale wachache walioboreshwa.

Ng’ombe walioboreshwa wamegawanyika katika makundi mawili, wale wanaofugwa kwa ajili ya nyama na wanaofugwa kwa ajili ya maziwa.  Ili kuwawezesha ng’ombe kuzalisha mazao bora ya nyama, maziwa na ngozi mfugaji anapaswa kufuata kanuni za ufugaji bora ambazo ni pamoja na:-

 1.  Kufuga ng’ombe katika eneo kwa kuzingatia uwianao wa idadi ya ng’ombe na malisho katika mfumo wa ufugaji huria.
 2. Kujenga banda au zizi bora.
 3. Kuchagua koo/aina ya ng’ombe kulingana na uzalishaji (nyama au maziwa).\
 4. Kutunza makundi  mbalimbali ya ng’ombe kulinga na umri na hatua ya uzalishaji.
 5. Kumpa ng’ombe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili.
 6. Kudhibiti magonjwa ya ng’ombe kama inavyoshauriwa na mtaalamu wa mifguo.
 7. Kuvuna mifugo katika umri na uzito muafaka kulingana na mahitaji ya soko.
 8. Kuzalisha maziwa, nyama na ngozi zinazokidhi viwango vya ubora na usalama.
 9. Kutunza kumbukumbu za uzalishaji na matukio muhimu ya ufugaji.

MIFUMO YA UFUGAJI
Ng’ombe wanaweza kufugwa katika mfumo wa ufugaji huria au kulishwa katika banda (ufugaji shadidi).  Ufugaji huria huhitaji eneo kubwa la ardhi yenye malisho mazuri na vyanzo vya maji.  Pamoja na kuwa na ufugaji huu, ni muhimu ardhi hiyo itunzwe kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya ng’ombe na malisho.  Ufugaji wa shadidi uzingatie uwepo wa banda bora na lishe sahihi.

UFUGAJI KATIKA MFUMO HURIA
Ili mfugaji aweze kupata mazao mengi na bora katika ufugaji huria anapaswa kuzingatia yafuatayo:-

1. Atenge eneo la kutosha la kufugia kulingana na idadi ya ng’ombe alionao.
2. Atunze malisho ili yawe endelevu na yapatikana wakati wote.
3.  Awe na eneo lenye maji ya kutosha na
4. Atenganishe madume na majike ili kuzuia ng’ombe kuzaa bila mpangilio.
5. Matunzo mengine ya ng’ombe yazingatie vigezo vingine muhimu kama umri hatua ya uzalishaji na matumizi ya ng’ombe husika.

MIPANGO KATIKA UFUGAJI WA NG’OMBE WA MAZIWA
Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo. Watu wengi ambao wanataka kuanzisha ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia. Kwa kawaida, wao wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata ng’ombe. Hapo ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza kwa kuwa ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.

Kwa wafugaji wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini kwake wanakuwa bado hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya ufugaji. Ili ujasiria mali kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa miundo mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta ng’ombe. Kwa mujibu wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika ya mashariki, ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:

 • Malisho bora na maji safi ya kunywa
 • Afya bora bila majeraha
 • Mazingira safi ikiwa ni pamoja na  banda lililojengwa vizuri
 • Uangalizi mzuri na wa kirafiki,  ambao humfanya ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.

Bila mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri, asitegemee kuwa ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa. Uzalishaji wa kiwango cha maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20% ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako vizuri naye atarudisha kwa kuzalisha maziwa vizuri.

PITIA
KICHAA CHA MBWA.

MIPANGO
Wafugaji ni lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe. Hii hujumuisha idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga, pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha malisho kinachohitajika kwa kipindi chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa kufahamu kuwa ni kwa namna gani malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.
Mfugaji ni lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa kipindi chote. Hii inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na kuhifadhi. Mipango ni nguzo muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya kufikia malengo yaliyokusudiwa, na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana mipango thabiti ni sawa na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari yake ni wapi.

MAHITAJI YA MLO KAMILI
Shughuli ya ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa uhusiano kati ya ulishaji wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato. Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.

MALISHO BORA
Tafuta ni aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako. Malisho endelevu hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na utunzaji wake shambani mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na hauwezi kumudu gharama za umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi kikubwa malisho ya wakati wa mvua na kuhifadhi ili kuweza kuyatumia wakati wa kiangazi.

Inashauriwa kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati wa mvua. Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye uweze kununua kutoka kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya mahindi, lusina, desmodiamu, na alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo hufanya vizuri katika maeneo mengi nchini Tanzania.

KIWANGO CHA KUTOSHA
Fahamu ni kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii itakusaidia kufahamu ni kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo 400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula kilo 12 za majani makavu kwa siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata malisho ya kutosha wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa kuzalisha maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18% ya malisho yote ni protini.

ZINGATIA UTUNZAJI NA UZALISHAJI WA MALISHO VIZURI
Wafugaji walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa gharama ya mbolea na mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia mbolea inayotokana na wanyama kupanda malisho na kuyatunza vizuri. Matete ni moja wapo ya malisho hayo. Endapo malisho hayo yatawekwa mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza kukupatia malisho ya mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.

WEKA MALISHO KATIKA HALI YA USAFI
Hifadhi malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua moja kwa moja, mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza kuyaharibu kama vile siafu na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini vya sumu vinavyoweza kuwepo kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora wa malisho kutokana na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye wingi wa majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu, shina kubwa na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia malisho yenye ukungu kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.

PITIA
IJUE TANGAWIZI NA FAIDA ZAKE

Kuweka kumbukumbu ni muhimu
Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji walio wengi. Baadhi ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi ya ziada, ambayo kulingana na wao haina uhusiano wowote na mapato yanayotokana na shughuli zao. Hata hivyo, bila uwekaji sahihi wa kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato kiasi gani anayopata kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji anaweza kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa

AINA YA NG’OMBE BORA WA MAZIWA
Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na ya kuvutia ambayo huwa na faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa yule anayependa kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara hata kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya kufuga. Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya jambo muhimu sana ambalo likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe wa maziwa kuwa na uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji.

Aina mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo kiwango cha maandalizi yako ni muhimu sana. Unahitajika kufahamu kuwa, unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji ya awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala hili limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa hujiingiza katika shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi yanayotakiwa pamoja na kuweka mipango thabiti.

Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya lishe na mambo mengine yako sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima kuzalisha kulingana na umbile lake na uwezo wake kamili. Kama utaweza kumudu kufuga ng’ombe halisi wa maziwa, ni lazima pia utambue kuwa uzalishaji wa juu wa maziwa uhitaji pia usimamizi wa hali ya juu. Kwa maana hiyo, ni vyema kufuga ng’ombe wa kiwango cha kawaida (ikiwezekana chotara) ambaye ataendana na uwezo wako wa kumtunza.

Kuna makundi mawili ya ng’ombe kuna wa nyama pamoja na wamaziwa. na kuna aina nyingine pia ni wazuri kwa nyama pamoja na wamaziwa mfano mpwapwa na sahiwal. hizi hapa na aina za ng’ombe wa maziwa

 •  Holstein Friesian
 • Brown swiss
 • Ayrshire
 • Guernsey
 • Jersey
 • Mpwapwa
 • Sahiwal
 • Red poll

(I) FRESHIANI (FRIESIAN)
Asili yake ni Holland, wanamabaka meupe na meusi, maziwa yao yana mafuta kiasi cha 3.5%, wanatoa maziwa mengi  6000 liters kwa kila msimu wa kukamua  watoto wake wanazaliwa wakiwa na 40 kg na zaidi., jike anauzito wa 400-600kg na dume 600-1000kgs   na urefu wa sentimeta 150 kutoka begani.
Ng’ombe aina ya freshiani ni rahisi kumtambua kutokana na kuwa na rangi nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama hawa ni wakubwa na pia wanaweza kuwa na mabaka meupe na meusi au mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa vizuri, freshian aliyefikia umri wa kukomaa huwa na uzito wa hadi kilogramu.

Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo wa kuishi kwa muda mrefu, uwezo wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni miaka sita. Hata hivyo, aina hii ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa maziwa ambao huweza kuzalisha kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa siku 360 yakiwa na kiwango cha chini cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ya ng’ombe.

PITIA
AINA MBALIMBALI ZA SUNGURA (RABBIT BREEDS)

Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji ulishaji mkubwa hivyo hushauriwa kwa wafugaji wenye uhakika wa kuwa na lishe bora na ya kutosha kwa mwaka mzima.

(II) AYRSHIRE
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany). Ng’ombe hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540 katika umri wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si rahisi kupata matatizo yeyote ya miguu.

Ayrshire huweza kufanya vizuri katika malisho ya aina yeyote tofauti na aina nyingine ya ng’ombe wa maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri na ulishaji mzuri, wastani wa uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa na kiwango cha juu cha mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni aina nzuri kwa kufuga hasa kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na uzalishaji mkubwa wa maziwa

Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa na umbo zuri pamoja na chuchu zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha, utungaji wa maziwa yake, umefanya maziwa yake kuonekana ni mazuri sana katika uzalishaji wa siagi na jibini.

Maziwa ya Ayrshire yanafahamika kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na uwezo wake wa kuwa na mafuta ya kutosha na kiasi kikubwa cha protini. Kwa mfugaji anayeanza, aina hii ya ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo kasha baadaye kuongeza freshiani baada ya uwezo wako wa kuhudumia kuwa imara.

Mifugo ya asili ni ghali sana na ni ngumu pia kuwapata, hivyo basi, njia rahisi kwa wafugaji wa maziwa wanaoanza ni kutafuta ng’ombe bora wa kawaida ambao mara nyingi huwa ni chotara, kisha kuwaboresha kwa kutumia mbinu ya kupandikiza dume bora na mwenye uzalishaji mkubwa. Na hii huhitaji elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi wa madume.

UCHAGUZI WA KOO NA AINA YA NG’OMBE WA KUFUGA
Kwa ufugaji wenye tija, mfugaji anashauriwa kuchagua koo na aina ya ng’ombe kwa kuzingatia malengo ya ufugaji (nyama au maziwa).

NG’OMBE WA NYAMA
Ng’ombe wanaofaa kufugwa kwa ajili ya uzalishaji nyama ni wale wanaokua kwa haraka na kuweka misuli mikubwa iliyojengeka vizuri.  Baadhi ya koo zenye sifa hizo ni pamoja na Boran, Mpwapwa (nyama na maziwa), Charolais, Aberdeen Angus, pamoja na chotara wao.  Hata hivyo, nchini Tanzania ng’ombe aina ya Zebu (mfano Ufipa,Gofo, Masai, Sukuma, Tarime, Iringa red), Sanga (Ankole) na chotara wao ndio hutumika kama ng’ombe wa nyama.

NG’OMBE WA MAZIWA.
Sifa za ng’ombe wa maziwa zifuatazo:-

(II) Umbo lililopanuka kwa nyuma na kupungua kuelekea kichwani.
(III) Mgongo ulionyooka kuanzia mabegani kuelekea mkiani
(IV) Miguu ya nyuma mirefu iliyonyooka, minene yenye kuacha nafasi kwa ajili ya kiwele na kwato imara.
(V) Kiwele kiwe kikubwa chenye chuchu nne, ndefu na unene wa wastani
(VI) Nafasi kati ya chuchu na chuchu iwe ya kutosha na
(VII) Endapo ng’ombe anakamuliwa awe na kiwele kikubwa kilichoshikamana vizuri mwilini, na mishipa mikubwa kwenye kiwele iliyosambaa.

Aina ya ng’ombe wa maziwa wanaofugwa kwa wingi nchini ni pamoja na Friesian, Ayrshire, jersey, Mpwapwa, Simmental na chotara watokanao na mchangoayiko wa aina hizo na Zebu.

Jiunge Nasi Telegram

Usipitwe na Nyaraka mpya kila zikiwekwa kwenye Tovuti yetu na weza kujifunza kwa kina ukitumia simu. Jiunge sasa hapa.

UFAHAMU MFUMO WA KILIMO SHADIDI

Mfumo wa kilimo shadidi cha mpunga (MKiShaMpunga) unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Sytem of Rice Intensification’ au ‘SRI’ kwa ufupi unajumuisha mbinu  vumbuzi za kilimo ambazo

Read More »