Tafiti mbalimbali zimetibitisha kwamba mmea huu kuwa na kiambato cha viuavijidudu, na ulianza kutumiwa kwa wingi na binaadamu sehemu mbalimbali unapopatikana ulimwenguni. Aina hizi za mmea huu zina maua yanayofanana ambayo yanaweza kuwa meupe au rangi ya zambarau na huwa na mbegu zinazofunikwa kwa maganda ambayo ni marefu na nyororo.
Kati ya aina zote za utupa ni aina moja tu ambayo kitaalamu hujulikanayo kama Tephrosia Vogelii ndiyo inayotambulika kuwa na kemikali iitwayo Rotanone yenye nguvu ya kuangamiza wadudu mbalimbali. Utomvu unaotokana na kukamuliwa mizizi ya mmea huu una asilimia 90 ya rotenone yote iliyopo kwenye mmea huu. Majani yake pia yanaweza kutumiwa kudhibiti wadudu waharibifu mashambani, kwenye maghala au wanyama wa majumbani. Faida kubwa ya dawa itokanayo na mmea wa Utupa ni kwamba:
• Haiharibui mazingira
• Sumu yake huisha baada ya siku tatu hadi tano baada ya kunyunyiziwa kwenye mimea.
Dawa hii imeonekana kufaa katika kudhibiti wadudu mbalimbali shambani, maghalani na kwa wanyama. Matumizi yake ni kama ifuatavyo:
KUDHIBITI WADUDU WAHARIBU MASHAMBANI:
• Vuna majani ya utupa, na wakati wa kuvuna hakikisha majani tu ndiyo yanayohitajika, pia izingatiwe kwamba iwapo majani yatavunwa vizuri mtini, itakuwa rahisi kwa majani mengine kuchipua haraka kwa ajili ya matumizi yake msimu unaofuata na pia itasaidia kuboresha hali ya udongo wa sehemu husika.
• Ili kupata utomvu ambao ndiyo wenye sumu ya maangamizo ya wadudu, inapasa kuyatwanga majani ya mmea huu kwenye kinu, na inapasa kutumia kilo moja ya majani kwa lita tano za maji ili kutengeneza sumu itakayokidhi lengo hili.
• Baada ya hapo yaache maji yajichanganye vizuri na utomvu utokanao na majani ya mmea huu. Uuache mchanganyiko huu kwa masaa mawili au unaweza kuchemsha mchanganyiko wa maji na majani kwa nusu saa.
• Kisha chuja mchanganyiko kwa kutumia kitambaa ili kupata juisi yake ambayo utaitumia moja kwa moja kunyunyizia mimea yako shambani. Unaweza kutumia nyunyizio lolote au bomba la mkono. Vilevile unaweza kuongeza kiasi kidogo cha sabuni ili kuzuia dawa hii isigande kwenye nyunyizio lako.
• Mchanganyiko unaweza ukatumika kudhibiti aina mbalimbali za wadudu kwenye, bustani za mbogamboga, mashamba makubwa, miti ya matunda na vitalu vya mimea. Ili kupata matokeo mazuri ni muhimu kuhakikisha dawa unayonyunyiza inamfi kia mdudu husika. Hata kama mdudu au wadudu watakuwa wamejifi cha chini ya majani, itabidi uhakikishe dawa imewapata vilivyo. Na baada ya kunyunyizia itabidi urudie tena zoezi hili baada ya siku saba. Vilevile kwa sehemu ambazo zimeathiriwa kiasi kikubwa na mchwa, majani ya utupa yanawezwa kusambazwa eneo lote.
KUDHIBITI WADUDU KWENYE MAGHALA:
Majani ya utupa pia yanaweza kutumika kutayarisha dawa yakudhibiti wadudu kwenye nafaka na jamii za maharage zinazohifadhiwa kwenye maghala na matayarisho yake huwa kama ifuatavyo:
• Vuna majani mabichi ya utupa na uyakaushe juani, yakishakauka uyatwange mpaka yageuke ungaunga.
• Baada ya hapo changanya ungaunga huu kwenye kilo 100 za nafaka yako, kama ni mahindi au maharage. Kwa kufanya hivyo utaweza kudhibiti wadudu wanaoshambulia nafaka hizi kama dumuzi na wengineo. Kinga hii huduma kwa miezi mitatu, iwapo utaendelea kuhifadhi nafaka zako basi inapasa kurudia zoezi la kuchanganya tena unga huu kwenye nafaka zako.
• Hakikisha unaosha vizuri nafaka zako kwa maji ili kuondoa ungaunga wa utupa kabla ya kutumia kwa chakula.
KUDHIBITI KUPE, CHAWA NA VIROBOTO KWENYE MIFUGO YETU
• Tayarisha dawa ya utupa kwa kuyatwanga majani kama ilivyoelezwa katika hatua ya kudhibiti wadudu waharibifu mashambani.
• Changanya kilo moja ya majani yaliyotangwa kwa lita tano za maji na baada ya hapo utaichuja mchanganyiko huu ili kupata juisi ambayo itatumika kumwogeshea mnyama. Tiba hii itamwondolea kabisa mnyama wako adha ya utitiri, chawa na viroboto .

TAHADHARI:
Sumu itokanayo na mmea wa Utupa ni hatari kwa samaki, binaadamu, wanyama wa nyumbani, na hata wa porini. Pia
usitumie utupa kuvulia samaki, kuvua samaki kwa kutumia mmea huu ni kinyume cha sheria sehemu mbalimbali duniani. Vilevile utumiapo utomvu utokanao na utupa weka mbali na ngozi yako au tumia glovu kama zinaweza kupatikana. Osha mikono kwa sabuni mara tu utakapomaliza kunyunyizia wanyama wako.